Asema, wakahojiwe, ni kwanini msitu wa hifadhi uvamiwe.
Mhe. Mkuu wa Wikaya ya Mwanga, Ndg. Thomas C. Apson, ameviagiza vyombo vya usalama kuwaweka ndani na kuwahoji M/Kiti wa Kijiji cha Kileo Ndg. Kazeni J. Mcharo na Mtendaji wa Kijiji hicho, Bi. Rista Sumpa, kwa kushindwa kusimamia msitu wa hifadhi wa Kileo, ambapo msitu huo, umevamiwa na watu wasiokuwa na moyo wa kizalendo wa kutunza mazingira na kusababisha uharibifu wa mazingira.
Akiwa ameongozana na kamati yake ya Ulinzi na Usalama, Mhe. Apson, amesikitishwa baada ya kushuhudia, eneo kubwa la hifadhi ya msitu huo, ambao ni sehemu ya chanzo cha maji, likiwa limekatwa miti huku kukiwa na zaidi ya matanuru 12, mengine yakiwa yanafuka moshi na mengine yakiwa kwenye hatua za kuwashwa moto kwa ajili ya kupata mkaa.
Katika kuhakikisha kuwa, uvamizi na uchomaji mkaa katika hifadhi ya msitu huo haiendelei, jumla ya watu nane wakiwemo wanaume 7 na mwanamke 1, wamekamatwa wakiwa ndani ya hifadhi ya msitu huo, wakiwa wanakata miti na kuchoma mkaa, na wamefikishwa polisi huku taratibu za kuwapeleka mahakamani zikiendelea. "Tunawapenda sana wananchi wetu, lakini kwenye makosa kama haya, watatusamehe, na ukiwaangalia hawa wahalifu, maisha yao ni ya chini, ila sheria lazima ifuatwe, alisema Mhe. DC."
Mhe. Dc ametoa wito kwa wananchi wa Kileo na Mwanga kwa ujumla kuwa, waache kuharibu misitu, kwani kufanya hivyo ni kuchezea mustakabali wa maisha yao wenyewe, sambamba na kuathiri uchumi wa nchi na maisha ya watanzania kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa