Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, leo limeketi na kufanya uchaguzi wa viongozi na wajumbe watakaounda, kamati mbalimbali ambazo zipo kisheria.
Uchaguzi huo ambao umefanyika chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Mhe. Theresia P. Msuya umefanikiwa kuunda jumla ya kamati nane ambapo kila kamati ina Mwenyekiti wake. Kamati hizo ni Kamati ya Fedha, Uongozi, na Mipango ambapo Mwenyekiti wake ni Mhe. Theresia P. Msuya, Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Mwenyekiti ni Mhe. Jeremia Shayo, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Mwenyekiti ni Mhe. Enea Mrutu.
Kamati zingine ni pamoja na Kamati ya Maadili, ambapo Mwenyekiti wake ni Mhe. Baraka Maradona, Kamati ya Ukimwi, Mwenyekiti wake ni Mhe. Fihiri Mvungi, Bodi ya Ajira ambayo mjumbe wake ni mmoja ambaye ni Mhe. Mwalim Ziad, ALAT wajumbe wawili ambao ni Mhe. Rodgers Msangi na Mhe. Kuria Msuya na kamati ya mwisho ni Ardhi yenye wajumbe wawili ambao ni Mhe. Aisha H. Salema na Mhe. BokaBakari S. Kuria.
Aidha Kamati hizi ambazo huwa zinaundwa na kuchagua uongozi wa kuziongoza, uchaguzi wake huwa unafanyika kila mwaka mpya wa fedha, hivyo kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 uundaji wa hizo kamati umefanyika leo. Sambamba na kuunda kamati hizo, Waheshimiwa Madiwani wamefanya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ambapo, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Mhe. Fihiri Msuya amechaguliwa tena kuendelea kuwa Makamu M/Kiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga.
Baada ya kamati kuundwa na viongozi wa kamati kupatikana,Mhe. Mwenyekiti wa Halmashauri aliwashukuru Waheshimiwa Madiwani kwa kuweza kushiriki vizuri kwenye kuwachagua Wajumbe na Wenyeviti wa kila kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti amewasisitiza na kuwaomba wajumbe wa kila kamati kuhakikisha kuwa, wanashiriki kwenye vikao ambavyo wao ni wajumbe ili waweze kutoa maamuzi sahihi na yenye tija kwa taifa.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa