Naibi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Kangi Lugola (MB) jana alifanya ziara yake Wilayani Mwanga na kuweza kutembelea kiwanda cha Kilimanjaro Biochem kinachojihusisha na uzalishaji wa spiriti na baadae kutembelea Ziwa Jipe ambalo linatumiwa na nchi ya Tanzania na Kenye.
Katika ziara yake hiyo ambayo aliambatana na maafisa mbalimbali wa Serikali wakiwemo Maafisa wa mazingira aliweza kukitembelea kiwanda cha Kilimanjaro Biochem na kujionea namna kiwanda hicho kinavyoendesha shughuli zake za uzalishaji. Sambamba na kujionea namna kiwanda hicho kinavyofanya kazi aliweza kukagua mazingira ya kiwanda na kutaka kujua kama wamiliki wa kiwanda wanafuata sheria za utunzaji wa mazingira kama sheria namba 20 ya mwaka 2004 inavyotaka.
Katika ukaguzi wake Mhe. Naibu Waziri aligundua kuwa maji taka ya kiwanda bado yana virutubisho vingi ambavyo ni hatari kwa mazingira na viumbe vyake kwa ujumla. Mhe. Naibu Waziri aliendelea kusema Serikali haita kaa kimya kama kiwanda hicho hakitaweka utaratibu na mfumo wa kutibu maji machafu na aliagiza mfumo wa kutibu maji hayo uwekwe ndani ya mwaka mmoja. “Natoa agizo kuwa mfumo wa kutibu maji machafu uwekwe na ukamilike ndani ya mwaka mmoja la sivyo kiwanda tutakifunga kama mtashindwa kutekeleza” alisema Naibu Waziri. Hata hivyo alisema maji machafu yanayotoka kiwandani hapo yana uwezo wa kuzalisha mbolea hivyo wamiliki wa kiwanda wafanye utafiti kwa kushirikiana na wataalamu kutoka chuo cha SUA ili waone ni namna gani mbolea hiyo inaweza kuzalishwa na kuweza kuwanufaisha watanzania.
Pamoja na dosari aliyoiona kiwandani hapo Mhe. Naibu Waziri hakuacha kutoa pongezi kwa Mkurugenzi wa kiwanda Ndg. Joshipura A.P kwa kuweza kutoa ajira zaidi ya 100 kwa wazawa na kuchangia miradi ya maendeleo kwa jamii inayozunguka kiwanda. Pia alitoa pongezi na shukrani kwa juhudi zilizochukuliwa na uongozi wa kiwanda kwa kuhakikisha kuwa hakuna hewa ya ukaa inayotoka kiwandani kitu ambacho ni kizuri katika utunzaji wa mazingira.
Akitoa shukrani zake kwa Serikali Mkurugenzi wa kiwanda cha Kilimanjaro Biochem Ndg. Joshipura A. P alisema “tumeyapokea maelekezo tuliyopewa na Mhe. Naibu Waziri na tunaahidi kwamba ndani ya mwaka mmoja tutayafanyia kazi kwani mwaka mmoja tuliopewa unatutosha”, alisema Ndg. Joshipura.
Akiwa ziwa Jipe Mhe. Naibu Waziri alijionea namna magugu maji yalivyosambaa katika ziwa hilo ikiwa sehemu kubwa ya magugu maji yapo upande wa Tanzania kuliko upande wa Kenya. Mhe. Naibu Waziri alisema kwa sasa kuna haja kubwa kwa Serikali kuhakikisha wanashughulika na magugu maji yaliyopo ziwa Jipe. Mhe. Naibu Waziri alisema mwaka 2017 Machi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba alitembelea Ziwa hilo na kujionea hali ilivyo hivyo anaamini ujio wao wote utakuwa siyo wa bure.
Mhe. Naibu Waziri alitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kuhakikisha kuwa wanatoa elimu kwa wananchi wanaoishi maeneo ya milimani ili wawe na kilimo cha uhifadhi ambapo wataepusha mmomonyoko wa udongo ambao unachangia ziwa kupungua kina. Pia alisema Mkurugenzi ahakikishe panakuwepo na kamati za mazingira kuanzia ngazi ya Kitongoji ili ziweze kusimamia na kuhakikisha hakuna uharibifu wa mazingira. Sambamba na hilo alisema Serikali kwa sasa inafanya operesheni kubwa juu ya uvuvi haramu hivyo wavuvi wajihadhari na uvuvi huo na wahakikishe wanakuwa na leseni za uvuvi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa