Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe ameahidi kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia miradi ya elimu na afya katika kata za Shighatini na Ngujini.
Ahadi hiyo ameitoa jana tarehe 24 Januari, 2022 alipokuwa katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi inayoendelea katika kata hizo. Miradi aliyoitembelea ni pamoja na mradi wa ujenzi wa maabara ya Biolojia katika shule ya Sekondari Kilobeni na mradi wa ujenzi wa maabara ya Fizikia katika shule ya Sekondari Ngujini. Miradi mingine ni pamoja na mradi wa ujenzi wa zahanati ya Vuchama Ndambwe na mradi wa ujenzi wa zahanati ya Chanjale.
Bi. Nasombe alisisitiza kwamba, fedha za kumalizia miradi hiyo zipo tayari na zinapelekwa kwenye taasisi husika ili ziweze kumalizia ujenzi wa miundombinu hiyo. Akifafanua kuhusu kiasi cha fedha kinachopelekwa kwa kila mradi Bi. Nasombe alisema, kiasi cha fedha kitakachopelekwa katika shule ya sekondari Kilobeni kwaajili ya kumalizia ujenzi wa maabara ya Biolojia ni shilingi milioni thelathini na shule ya sekondari Ngujini itapelekewa kiasi kama hicho kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa maabara ya Fizikia.
Kwa upande wa Zahanati alisema kwamba, Zahanati ya Vuchama Ndambwe itapelekewa kiasi cha shilingi milioni hamsini kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa zahanati hiyo. Aidha zahanati ya kijiji cha Chanjale ipo katika hatua za mwisho za umaliziaji. Mwaka wa fedha wa Serikali uliomalizika mwaka 2020/2021, zahanati hii ilipokea kiasi cha fedha za kitanzania shilingi milioni hamsini fedha ambazo bado zinaendelea kutumika katika kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi amewasisitiza na kuwataka wasimamizi wa miradi hiyo hususani katika ngazi ya Kijiji na Kata kuhakikisha kuwa, nguvu za wananchi zinakuwepo kwenye ujenzi ili waone thamani ya nguvu kazi yao kwenye miradi iliyopo kwenye maeneo wanayoishi
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa