Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, ametoa maelekezo kwa mkandarasi anayesimamia mradi wa maji safi wa Mwanga-Same-Korogwe kuhakikisha kuwa, mradi huo unakamilika kwa wakati.
Ametoa maelekezo hayo leo, alipotembelea Wilaya za Mwanga na Same kujionea namna shughuli zinavyofanyika kwenye mradi huo. Amesema kwamba, mradi huo umechukua mda mrefu hivyo unatakiwa uishe kwa haraka. Ameendelea kusema kuwa, atahakikisha fedha inayochangiwa na Serikali kwenye mradi huo inatoka mapema ili kuufanya mradi uende kwa kasi zaidi.
Mradi wa Mwanga-Same-Korogwe ni moja kati ya miradi mikubwa nchini inayojengwa ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaondokana na adha ya maji hapa nchini. Mradi huu utagharimu kiasi cha dola za marekani milioni 41.35. Baada ya mradi kukamilika utanufaisha wananchi wa Wilaya tatu ambazo ni Mwanga, Same na Korogwe.
Aidha Katika ziara yake hiyo, ametoa maelekezo kwa wakala wa uchimbaji visima (DDCA) kuhakikisha kwamba, wiki ijayo anakuja Wilayani Mwanga kuendelea na mradi wa kuchimba visima vilivyopo Usangi, ambavyo, wakala huyo alikuwa hajavimalizia toka mwaka jana.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri ameelezwa namna Wananchi wa Mji wa Mwanga wanavyopata shida ya maji kutokana na kukatiwa umeme na TANESCO. Kufuatia taarifa iliyosomwa kwake na, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Ndg. Golden A. Mgonzo, ameelezwa kwamba, Mamlaka ya Maji ya Mji Mdogo Mwanga imekuwa ikikatiwa maji mara kwa mara kutokana deni la shilingi, milioni 211.7 deni ambalo ni la miaka mingi. Mhe. Waziri ameombwa Wizara yake isaidie kulipa deni hilo kwani Mamlaka ya Maji Mwanga haitakuwa na uwezo wa kulipa. Mhe. Waziri ameahidi atalifuatilia jambo hilo na kujua ni kwa namna gani linaweza likatatuliwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa