Leo tarehe 08.12.2021 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga imefanya maadhimisho ya sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika pamoja na miaka 59 ya Jamuhuri. Maadhimisho hayo yamefanyika siku moja kabla ambapo kilele cha maadhimisho kitaifa yanategemea kufanyika hapo kesho tarehe 09.12.2021.
Katika maadhimisho hayo ambayo yaliambatana na kauli mbiu isemayo "Tanzania yenye Uchumi Imara na Maendeleo ya Viwanda kwa Ustawi wa Taifa Letu" yaliongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mwanga Ndg. Amini Mrisho. Akihutubia wananchi waliofika katika maadhimisho hayo, Ndg. Mrisho amesema, nchi ya Tanzania imepiga hatua kubwa toka ipate uhuru wake kwani yapo mambo mengi ya kuonekana kama elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa kidato cha kwanza hadi cha nne na uwepo wa shule za sekondari ambapo kwa asilimia kubwa, kata karibia zote zina shule za sekondari.
Ndg. Mrisho ameendelea kusema kuwa, serikali ya Tanzania imeendelea kuimarisha muungano, ujenzi wa vituo vingi vya afya ili kusogeza huduma karibu na wanachi, biashara imeimarika pamoja na kuimarika kwa ulinzi na usalama wa nchi. Akielezea hatua nyingine ambayo Tanzania imepata toka iachane na utumwa ni pamoja na kufanikiwa kuondoa kila aina ya ubaguzi pamoja na ukabila ambapo Tanzania ni nchi yenye makabila mengi lakini iliweza kuunganishwa kwa lugha ya Kiswahili.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa