Operesheni ya kukabiliana na uvuvi haramu, inayofanywa na wizara ya Mifugo na Uvuvi katika bwawa la Nyumba ya Mungu, lililoko Wilayani Mwanga, imeweza kuiingizia serikali kiasi cha Tsh. 95,720,000. Hayo yamesemwa na Kamanda wa operesheni ya kutokomeza uvuvi haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu Ndg. Ranwel Mbukwah.
Akisoma taarifa ya operesheni hiyo, mbele ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Hamisi Ulega, kamanda huyo alisema, kiasi hiki cha mapato ambacho ni kiasi kikubwa ndani ya muda mfupi kimetokana na faini mbalimbali walizotozwa, wavuvi ambao wamekamatwa wakiwa wanajihusisha na uvuvi haramu. Operesheni hii ambayo ilianza tarehe 18 Octoba, 2018 imekuwa ya manufaa sana, kwani jumla ya watuhumiwa 84 wamekamatwa na kati ya hao, watuhumiwa 83 wamelipa faini na mtuhumiwa mmoja ameshindwa kulipa faini na yupo kwenye vyombo vya sheria, pikipiki zinazofanya biashara haramu zimekamatwa, na samaki wachanga wameweza kuteketezwa.
Baada ya kupata taarifa hiyo ya operesheni, Mhe. Naibu Waziri aliweza kuongea na kuwahutubia wavuvi wa kijiji cha Kagongo, na baadae kufanya zoezi la kuteketeza nyavu haramu ambazo zilikamatwa kabla na wakati wa zoezi hili la operesheni ya kutokomeza uvuvi haramu. Akiongea na wananchi hao alisema, wavuvi wanapaswa kulinda bwawa lao kwa manufaa ya vizazi vya baadae. Ameendelea kusema, anasikitishwa na kitendo cha kuona Supermarket zikiwa zinauza samaki kutoka nje ya nchi wakati, tuna uwezo mzuri wa kulinda na kuachana na uvuvi haramu. Amesema, uvuvi endelevu una manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na super market zetu kuuza samaki wetu wenyewe. Pia amesema, wavuvi wanapaswa kuthaminiwa, kwani nao wana mchango wa moja kwa moja kwenye katika kukuza uchumi wa nchi.
Mhe. Naibu Waziri hakuacha kutoa onyo kali kwa wale ambao bado wanaendelea na uvuvi haramu. Amesema, serikali haitakuwa na huruma na mtu yeyote anayevua kwa njia haramu ama mtu anayefadhili shughuli za uvuvi haramu na amesema kuwa, operesheni inayoendelea sasa ni endelevu. Pia amewataka wananchi wanaolima kandokando ya bwawa, kuacha shughuli hiyo mara moja. Amesema, kilimo kinachoendelea kandokando mwa bwawa, kinapelekea bwawa kupungua kina siku hadi siku.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa