FURSA YA UWEKEZAJI KWENYE KILIMO
Sehemu kubwa ya wakazi wa Wilaya ya Mwanga, kazi wanayo jishughulisha nayo ni kilimo, ufugaji na uvuvi. Kahawa na zao la ndizi zinalimwa maeneo ya milimani ambako mvua huwa ni za uhakika zaidi kuliko maeneo ya tambarare. Pia maeneo ya milimani wanatumia maji ya umwagiliaji ambayo huwa yanafahamika zaidi kama maji ya ndiva. Kwa upande wa maeneo ya tambarare ya mashariki, kaskazini na magharibi mvua huwa ni kidogo sana hivyo maeneo haya kilimo cha umwagiliaji ndicho kinacho limwa zaidi. Maeneo haya yanalimwa zaidi zao la mahindi, maharage, vitunguu na mpunga.
Zao kubwa linalo limwa Wilayani Mwanga ni Mahindi, fiwi, mpunga, ndizi, kahawa, matunda na mbogamboga. Kwa wastani kila mwaka uzalishaji wa mahindi ni tani 6,500, mpunga tani 350, maharage tani 1,100, maparachichi tani 3,000, ndizi tani 15,000 na kahawa ni tani 90.
Wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali wanakaribishwa Wilayani Mwanga kutumia fursa na rasili mali ya ardhi iliyopo ili waweze kuwekeza kwenye kilimo kwani ardhi ipo ya kutosha.
Maeneo ambayo yanatoa fursa ya uwekezaji wa kilimo ni pamoja na;
Kilimo cha umwagiliaji Kirya, Kileo na Kivulini. Kuna jumla ya hekta 900 za umwagiliaji kwenye Kata ya Kirya ambapo, hadi sasa hekta 150 tu ndizo ambazo zinatumika. Wawekezaji wanakaribishwa kuja kuendeleza hekta zilizo baki ambazo zina rutuba nzuri na hali ya hewa nzuri inayo ruhusu kilimo cha Umwagiliaji kwenye eneo hili. Eneo lingine ambalo linafaa sana kwa kilimo cha umwagiliaji ni Kijiji cha Kileo chenye jumla ya hekta 2,400 ambazo zinafaa kulimwa kwa kipindi chote cha mwaka. Kijiji cha kivulini kina jumla ya hekta 1,050 ambapo, hekta zinazotumika kwa kilimo ni 400 tu. Tarafa ya Jipe Ndea nayo ni miongoni mwa maeneo yenye ardhi ya kutosha inayo faa kwa kilimo. Maeneo yote haya yanafaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali kama alizeti, mtama, uwele, miwa, mahindi, maharage, fiwi/ngwara, korosho, mbogamboga, matunda na mpunga kwa maeneo ya Kirya na Kileo.
Maeneo ya kujenga viwanda vya kusindika mazao. Kutokana na uwepo wa maeneo mengi ya kulima mazao ya aina tofauti, Wilaya inawakaribisha wawekezaji wenye nia ya kuanzisha viwanda vya usindikaji wa mazao kama kahawa, alizeti, mpunga,mahindi na mazao ya matunda na mbogamboga.
Kuanzisha maduka ya pembejeo za kilimo. Mazao mengi yanapokuwa shambani yanahitaji viwatilifu ili kuuwa wadudu wanao shambulia mazao. Pia wakulima wanahitaji pembejeo mbalimbali za kutumia shambani kama mbolea na mbegu. Kwasababu hii wakulima wanapata shida ya kupata pembejeo kwa wakati kutokana na kufuata madawa kwenye maduka yaliyoko mbali na eneo la kilimo. Hivyo hii ni fursa nzuri kwa wazawa na wasio wazawa kuja kuwekeza Mwanga na kuweza kuanzisha maduka ya pembejeo za kilimo ili kuwarahisishia wakulima kwenye huduma ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
Fursa nyingine iliyopo kwenye sekta ya kilimo ni pamoja na uwepo wa maeneo ya kuchimba mabwawa ya kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na ujenzi wa masoko ya mazao mbalimbali kwenye Kata za, Kileo, Mwanga, Mgagao na Lembeni.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa