CHIMBUKO/ASILI YA WILAYA YA MWANGA
Wilaya ya Pare ilikuwa inaongozwa na Machifu tisa (9) ambao kwa umoja wao walikuwa wanabadilishana uongozi kila baada ya mwaka mmoja.
Machifu hao ni kama ifuatavyo.
Machifu hawa walifanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya wakoloni. Ili kuimarisha ulinzi katika eneo la hawa machifu palikuwa na walinzi waliokuwa wakiitwa Wachili, pamoja na kazi zao walihakikisha kuwa Chifu anakuwa katika hali ya usalama hivyo walipewa maeneo ya kuishi jirani na machifu. Kazi mojawapo ya Machifu ilikuwa ni kukusanya kodi ( Poly Tax ). Hata hivyo mnamo miaka ya hamsini machifu walishindwa kukidhi haja ya wakoloni hivyo chini yao wakaanzishwa Walao ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kukusanya kodi. Kwa kipindi hiki badala ya walao ni Makatibu Tarafa. Enzi za machifu palikuwa na Area Commissioner (AC) ambao kwa namna nyingine waliitwa Bwana shauri kwani hao ndio walikuwa ni Mahakimu katika ngazi ya wilaya.
MAKABILA/LUGHA.
Wilaya ya Pare tangu zamani ilikuwa na wakazi wenye lugha mbili ( 2), kwa Pare zote za Kusini na Kaskazini lugha kuu ni Kipare. Kwa Pare ya Kaskazini na hususani maeneo ya Ugweno iko lugha kuu ya Kigweno, yenye lafudhi inayoendana zaidi na Kichagga kuliko Kipare.
WILAYA YA MWANGA. (1979 – MPAKA SASA).
Wilaya ya Mwanga ilianzishwa tarehe 1, Julai,1979 baada ya Uhuru wa Tanganyika, kwa hivi sasa ni miongoni mwa wilaya Sita (6) za Mkoa wa Kilimanjaro, wilaya nyingine ni pamoja na Same, Rombo, Hai, Moshi na Siha. Wakati wa kuanzishwa ilikuwa miongoni mwa wilaya nne (4) ambazo zilikuwa Same, Moshi na Rombo, kabla ya kuanzishwa kwa wilaya mpya za Hai na Siha.
UTAWALA
Wakati wa kuanzishwa Wilaya ya Mwanga ilikuwa na Tarafa 4 za Mwanga, Ugweno, Usangi na Lembeni kabla ya kuanzishwa Tarafa mpya ya Jipe Ndea. Wilaya ilikuwa na Kata 16, Vijiji 53, na Jimbo moja la uchaguzi. Kwa sasa Wilaya ina Tarafa 5 za Jipe Ndea, Mwanga, Lembeni, Usangi na Ugweno na ina Mamlaka ya Mji Mdogo 1 yenye Vitongoji 12. Wilaya ina Kata 19 za Mgagao, Lembeni, Kileo, Lang’ata, Kirya, Kivisini, Kwakoa, Toloha, Mwaniko, Kifula, Msangeni, Shighatini, Kighare, Chomvu, Ngujini, Kilomeni, Kigonigoni, Kirongwe na Jipe, kuna vijiji 72 na Vitongoji 272.
UKUBWA WA ENEO
Ukubwa wa eneo la Wilaya ni kilomita za mraba 2641 kati ya hizo eneo la ardhi ya nchi kavu ni kilometa za mraba 2,558.6 na eneo la maji ni kilometa za mraba 82.4 ambapo Km 52 za mraba ni eneo la maji ya bwawa la Nyumba ya Mungu na Km 26.4 za mraba ni eneo la maji ya Ziwa Jipe.
WATU NA MAKAZI
Wakati inaanzishwa Wilaya ya Mwanga mwaka 1979 ilikuwa na wakazi wapatao 74,620 na kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2022 Wilaya ilikuwa na idadi ya watu 148, 763, ambapo wanaume walikuwa 72,157, na wanawake walikuwa ni 76,606, na jumla ya kaya zilikuwa ni 38,847.
HALI YA HEWA.
Wilaya inapata mvua kati ya millimita 400- 600 kwa maeneo ya Nyanda za Chini na kati ya millimita 800-1,200 kwa maeneo ya Nyanda ya Juu. Kuna misimu miwili ya mvua Vuli na Masika. Vuli huanza mwezi Oktoba hadi Desemba na Masika huanza mwezi Machi hadi Juni. Maeneo ya Nyanda ya Juu hupata mvua zote za Vuli na Masika. Wilaya hupata upepo mkali unao vuma tokea upande wa Mashariki kuelekea Magharibi, kiwango cha joto ni kati ya Nyuzi 14 sentigredi hadi Nyuzi 32 sentigredi hasa kwa mwezi Januari.
SHUGHULI ZA KIUCHUMI
1. KILIMO.
Kwa upande wa tambarare ya Mashariki na Magharibi kuna kilimo cha umwagiliji ambapo zao maarufu ni mahindi na mpunga kwa ajili ya biashara.
Asilimia 85 ya wananchi wanaishi vijijini. Uchumi wa wilaya unategemea sana kilimo, ufugaji, uvuvi na sehemu ndogo wanajishughulisha na biashara ndogo ndogo. Mazao makubwa ya biashara yanayolimwa ni Kahawa,na Mkonge . Mazao ya chakula ni Mahindi, Maharage, Ndizi, Mihogo, Viazi vitamu na Mpunga.
2. UFUGAJI.
Ufugaji unakwenda sambamba na kilimo kwani unachangia Wananchi kuinua kipato chao. Kwa takwimu za mwaka 2016/17 Wilaya ina idadi ya Ng’ombe 117,007 wa kisasa wakiwa 14, 398 na kienyeji wakiwa 102, 609, Mbuzi 151,109, Kondoo 67, 102, Nguruwe 616, Sungura 196, Kuku 252 200, na Bata 2, 340, Punda 1, 317, Ngamia 8. Mifugo hii huuzwa kwa ajili ya kujipatia kipato. Pia Ng’ombe hutoa maziwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kuuza ili kupata fedha za kujikimu kimaisha, na ngozi huuzwa katika masoko ya ngozi ndani na nje ya Wilaya na kuongeza mapato ya Wafugaji.
3. UVUVI.
Kuna shughuli za Uvuvi katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ambao ulianza mwaka 1969 baada ya Bwawa kujengwa. Pia kuna shughuli za uvuvi katika Ziwa Jipe ambapo wavuvi pamoja na wananchi katika maeneo hayo hujipatia mapato kutokana na uvuvi na biashara ya uvuvi. Samaki wanaovuliwa huuzwa ndani na nje ya Wilaya ya Mwanga.
4. BIASHARA.
Wilaya ina idadi ya biashara zifuatazo:- Baa na ‘’Grocery’’160, Maduka ya rejareja na Vioski 520, Maduka ya jumla 3, Mikahawa 80, Gereji 5 ,Hotel 1, Motel 6, Nyumba za kulala wageni 18, na kuna Vituo vya Mafuta 4 vinavyofanya kazi, na maduka ya hardware 14.
5. UFINYANZI.
UONGOZI WA WILAYA YA MWANGA BAADA YA UHURU
Baada ya kuondolewa kwa utawala wa Machifu mwaka 1963, uongozi wa kiwilaya uliwekwa chini ya Wakuu wa Wilaya. Wakuu wa Wilaya (Area Commissioner) katika Wilaya ya Pare toka mwaka 1962 hadi 1979 walikuwa wafuatao:-
Na. |
Jina la Wakuu wa Wilaya |
Muda |
1 |
BWANA AMSIRONG ( MZUNGU)
|
1962 |
2 |
KAUGAHUA
|
1962 – 1963 |
3 |
MBWANA KIHERE
|
1963 – 1965 |
4 |
J. GWAHU
|
1965 – 1967 |
5 |
MADENGE
|
1967 – 1969 |
6 |
RWECHUNGURA
|
1969 – 1972 |
7
|
NYEMELE
|
1972 – 1975 |
8
|
MWAKATOBE
|
1975 - 1979 |
ORODHA YA WAKUU WA WILAYA TOKA WILAYA YA MWANGA ILIPOANZISHWA MWAKA 1979
NA.
|
JINA KAMILI |
MWAKA ALIOANZA |
MWAKA ALIO ONDOKA |
1
|
Bi Salome Philemoni Nyiti
|
1979 |
1980 |
2
|
Bw. Adolfu Abeli Mwakyusa
|
1980 |
1981 |
3
|
Bw. Pius Mkongoti
|
1981 |
1986 |
4
|
Bw. B. K. Sanga
|
1986 |
1992 |
5
|
Capt. T. L.A. Mwabeza
|
1992 |
1997 |
6
|
Bw. John Tuppa
|
1997 |
2001 |
7
|
Bw. Rubeni Ole – Kuney
|
2001 |
2005 |
8
|
Bw. Jordan O. Rugimbana
|
2005 |
2009 |
9
|
Bw. Athumani Hassani Mdoe
|
2009 |
2011 |
10
|
Shaibu I. Ndemanga
|
2012 |
2016 |
11
|
Aaron Y. Mbogho
|
2016 |
2019 |
12
|
Thomas Cornel Apson
|
2019 |
2021 |
13
|
Abdallah Mussa Mwaipaya
|
2021 |
Mpaka sasa |
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa