Wilaya ya Mwanga ni miongoni mwa Wilaya zinazo vutia Mkoani Kilimanjaro kutokana na aina mbalimbali za vivutio vya utalii vinavyopatikana hapa Wilayani. Kutokana na uwepo wa vivutio vingi vya utamaduni na mali asili, fursa za uwekezaji zinapatikana kwa watanzania wazawa pamoja na wageni kutoka nje ya nchi ili kuwekeza kwenye utalii kwa manufaa yao na kwa manufaa ya Wilaya ya Mwanga.
Wilaya ina eneo lenye ukubwa wa Kilomita za Mraba 2641; Kutokana na uwepo wa maeneo ya kutosha, wawekezaji wanaweza kuanzisha Makambi ya watalii ama hoteli. Mfano maeneo ya tambarare ni mazuri kwa kuwekeza kwa kujenga hoteli ama makambi ya watalii. Pia maeneo ya bwawa la Nyumba ya Mungu na ziwa Jipe ni maeneo mazuri sana yanayo faa kwa wawekezaji. Maeneo haya yatatoa fursa nzuri kwa watalii wanaopenda utalii wa kuvua na kuogelea.
Maduka makubwa ya biashara na hoteli yanafaa sana kuanzishwa wilayani Mwanga kwani Wilaya ina takribani watu 115,145 (kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002), pia wilaya ipo kwenye barabara kuu kuelekea mjini Moshi na Jiji la Arusha ambapo maeneo haya ni ya Kitalii. Hivyo, maduka makubwa na hoteli vikiwekezwa hapa Mwanga itakuwa ni fursa nzuri kwa watalii kabla ya kufika maeneo yenye vivutio vya kitalii.
Pamoja na fursa za uwekezaji zilizotajwa hapo juu, pia kuna maeneo mengi yenye vivutio vya utalii hapa wilayani ambapo maeneo haya yanafaa kuwekezwa kwa shughuli za utalii. Kwa kutembelea maeneo haya itakuwa ni fursa nzuri ya kupata elimu kwa wale wanaotaka kuwekeza Mwanga hususani kwenye sekta ya utalii. Wawekezaji wanahimizwa kuja kutembelea kwenye maeneo haya ya utalii ili kuchagua maeneo mazuri ya kuwekeza.
Milima ya Pare, maarufu kwa jina la Eastern Arc Mountains (Tawo la mashariki). Maeneo ya Vuchama Ndambwe,
Watalii wakiwa maeneo yaVuchama Ndambwewataona kwa uzuri mandhari ya Bwawa la Nyumba ya Mungu, mashamba ya katani ya Kisangara na Lembeni, Mlima Kilimanjaro na makazi ya watu
Katika maeneo ya Mangatu, Ndandana Milima ya Ngofi watalii wataweza kuona upande wa mashariki ambapo, watafurahia kuona Ziwa Jipe, Kivisini na tambarare ya nchi jirani ya Kenya na makazi.
Misitu ya asili na misitu ya hifadhi (Mingine ipo chini ya Serikali na mingine ipo chini ya Koo).
Msituwa hifadhi wa Mlima Kindoroko ni sehemu ambapo watalii wanaweza kutembelea na kuona kima weusi, vipepeo, ndege na mimea ya aina mbalimbali.
Msitu wa hifadhi waMinja, Kamwala I na Kamwala IIni maeneo mengine ambapo kuna miti ya asili, vipepeo, wanyama wadogowadogo, na ndege wa aina mbalimbali. Misitu ya ukoo(Mpungi). Misitu ya ukoo/koo ni aina ya misitu inayomilikiwa ama kutunzwa na koo. Aina hii ya misitu ipo sehemu mbalimbali kama Ugweno, Usangi na Tarafa ya Lembeni.
Katika kata ya Kileo, kuna msitu wa hifadhi wa Kileo ambao una chemchem mbili ambazo ni vyanzo vya maji, chemchem hizo ni Mtindi na Ivonokwaambapo chanzo cha chemchem hizo ni mto wa chini ya ardhi unaoanzia Mlima Kilimanjaro.
Maeneo ya Kihistoria/Historia (Historical sites):Kuna maeneo mengi ya kihistoria hapa Wilayani Mwanga. Maeneo hayo ni pamoja na;
Milima ya Ngofi; Kihistoria, milima ya Ngofi ilikuwa kama njia ya baadhi ya makabila kutoka Kenya kuja sehemu za Upareni.
Kikweni:Eneo la Kikweni ni eneo ambalo lilikuwa linawaunganisha watu wa Ugweno na Usangi. Eneo hili pia lilitumika kama eneo la kuwaadhibu wale waliokamatwa wakifanya uzinzi kabla ya kuoana. Waliokamatwa wakifanya uzinzi walifungwa pamoja na kuachwa eneo hilo mpaka kufa, na hii ilifanyika ili kila mtu aone kuwa ni sehemu ya laana.
Maporomoko ya Yefukana shamba la Yefuka;Viunga vya maji kutoka Usangi na Ugweno imeungana na kuunda maporomoko ya Yefuka. Maporomoko haya yametengeneza bwawa la asili ambalo linaweza kutumika kama sehemu ya kuogelea. Shamba la Yefuka nalo ni eneo lililotunzwa vizuri na kuwa na mandhari ya kuvutia. Eneo hili lina vivutio kama; nyani, ndege, vipepeo, mimea ya aina mbalimbali, pia wageni watapata fursa ya kutembelea na kuona maeneo ambayo watoto wadogo waliozaliwa wakiwa na aina fulani ya ulemavu walitupwa .Ndani ya shamba la Yefuka kuna mtaalamu anayehusika na matibabu kwa kutumia miti shamba. Watalii watapata fursa ya kupatiwa elimu juu ya matibabu kwa kutumia miti shamba. Pia kwa watalii wanaohitaji kuweka mahema (camping),Yefuka Farm ni sehemu nzuri kwa wageni kama hao.
Makumbusho ya Mkumbavana;Hii ni makumbusho ya kipekee na ya muhimu iliyopo hapa Wilayani Mwanga, kwani inatumika kama sehemu ya kupatia historia na elimu kuhusiana na watu wa Mwanga na shughuli zao za kiuchumi. Makumbusho hii inatoa fursa ya kujifunza tamaduni za kipare, kuona zana za asili za zamani, mapango na miamba ya kutengeneza (isiyo ya asili), inayo onyesha picha halisi ya mazingira yanayozunguka milima ya Pare, uchezaji wa ngoma halisi ya kipare,kuona na kula chakula cha asili, kupanda mlima na kufikia eneo la mkumbavana (eneo walipotupwa watoto waliozaliwa wakiwa na ulemavu), kutembelea eneo la makaburi ya ukoo.
Kanisa la kwanza la Wamisionari Wilayani Mwanga;Kanisa la K.K.K.T la Shighatini ndilo kanisa la kwanza kuanzishwa na wamisionari Wilayani Mwanga. Kanisa hili lilijengwa mwaka 1900 na bado linatoa huduma kwa waumini mpaka leo na karibu na kanisa, kuna kaburi la mmisionari wa kwanza kufika katika eneo hilo.
Kutembelea maboma ya wamasai na kuona ngoma za asili, zoezi hili linaweza kuratibiwa kulingana na uhitaji wa watalii.
Bwawa la Nyumba ya Mungu, Ziwa Jipena Mto Pangani
Ziwa JipeKatika ziwa Jipe wanyama kama kiboko, swala, tembo nk wanapenda kukusanyika kandokando mwa ziwa hususani, wakati wa asubuhi kwa ajili ya kupata maji. Pia utalii wa boti kwa kutumia boti za asili (boti za wavuvi), unaweza kuratibiwa katika ziwa Jipe.
Bwawa la Nyumba ya Mungu;Bwawa la Nyumba ya Mungu ni bwawa ambalo limezungukwa na watu ambao, kipato chao cha kila siku wanakipata kutoka kwenye bwawa hili kwa njia ya uvuvi.Shughuli za kitalii ambazo zinaweza zikaandaliwa katika bwawa la Nyumba ya Mungu ni pamoja na utalii wa boti kwa kutumia boti za wavuvi, utalii wa safari kwa kutumia ngamia, kambi za kitalii (camping safari) nk.
Mto Pangani; Mto huu ni miongoni mwa mito mirefu hapa Tanzania, na unapita Wilaya ya Mwanga kwa umbali wa KM 32.
Utalii wa kupanda milima;Katika Wilaya ya Mwanga, kuna milima miwili ambayo inaweza ikafikika na kupandwa kwa urahisi; Milima hiyo ni Kindoroko na Kamwala. Mtalii/watalii wakithitaji kupanda milima hii, mara nyingi safari ya kuanza kupanda huwa inaanzia Usangi mpaka kilele cha Mlima Kindoroko na Kamwala. Milima hii ni shemu nzuri ya kumuweka mtalii vizuri kabla ya kupanda milima mikubwa kama Mlima Kilimanjaro na Mlima Meru.
Kambi za watalii (Camping Sites): Kuna maeneo mengi ambayo kambi za watalii zinaweza kuanzishwa,kwa kutegemea na aina ya utalii ambao wahusika wanataka kufanya. Mfano, sehemu ya milimani kuna maeneo kama Kamwala, Ndorwe na Vuchama Ngofi. Sehemu ya tambarare kuna maeneo kama Lang’ata, shamba la Yefuka, Jipe nk.
Utalii wa Kilimo na ufugaji: Shughuli kuu za kiuchumi za watu wa Mwanga ni kilimo, ufugaji na uvuvi. Mazao ya kahawa na ndizi yanalimwa zaidi maeneo ya ukanda wa milimani ambapo pana uwepo wa mvua za kuridhisha. Kutokana na uwepo wa mvua chache ukanda wa tambarare, mfano Kirya na Kileo, kilimo cha umwagiliaji ndicho kinacholimwa zaidi kwa mazao kama mahindi, mpunga na mazao ya jamii ya kunde.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa