Ikiwa imebaki miezi miwili kufunga mwaka wa Serikali wa 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga imefanya vizuri sana kwa kuweza kukusanya mapato kwa asilimia 99.09. Hii ni ishara kuwa, Halmashauri imesimama vizuri kwenye kusimamia mapato ya Serikali hususani mapato ya ndani.
Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 iliyokuwa imetengwa na Halmashauri ni Tsh. 2,150,130,000.00 ambapo hadi kufikia wiki ya kwanza ya mwezi mei, Halmashauri ilikuwa imeshakusanya kiasi cha Tsh. 2,130,648,266.99 sawa na asilimia 99.09. Kwa makusanyo haya, hadi kumalizika kwa wiki ya pili ya mwezi mei, Halmashauri itakuwa imeshafikia lengo lake la kukusanya mapato ya Tsh. 2,150,130,000 sawa na asilimia 100.
Akiwa anaeleza sababu zilizopelekea kufikia asilimia hizi, wakati kukiwa bado kuna miezi miwili ya kuendelea kukusanya mapato kwa mwaka 2017/18, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Ndg Golden A. Mgonzo amesema, Halmashauri imeweza kufikia asilimia hizo kwasababu ya usimamizi mzuri unaofanywa na ofisi yake. Ameendelea kusema kuwa, kazi kubwa na nzuri imeendelea kufanywa na kikosi kazi chake alichokiunda cha kufuatilia na kukusanya mapato ya Halmashauri. Mkurugenzi ameendelea kueleza kwamba, Bwawa la Nyumba ya Mungu, huwa ni sehemu ya chanzo muhimu sana cha kuiingizia Halmashauri mapato lakini Bwawa hili lilifungwa kwa miezi sita. Japokuwa Bwawa hili limefungwa, bado Halmashauri imeendelea kukusanya mapato yake vizuri na kupelekea kufikiwa hizo asilimi, alisema Mkurugenzi.
Akieleza sababu zingine zilizopelekea kufikia kiwango kikubwa cha ukusanyaji wa mapato, alisema, mapato ya ushuru wa huduma kwa mteja na mapato ya vibali vya ujenzi yalikuwa hayakusanywi vizuri. Lakini toka yaanze kufuatiliwa kwa ukaribu na kikosi kazi cha mapato, Halmashauri imeendelea kukusanya fedha nyingi kutoka kwenye hivi vyanzo.
Kwa kiwango hiki kilichofikiwa na Halmashauri ni ishara tosha kuwa Serikali iliyoko madarakani inaendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu mkubwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa