Siku za karibuni imeripotiwa kuwa, umetokea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, kwa baadhi ya maeneo ya Halmashauri ya Moshi iliyoko Mkoani Kilimanjaro, na baadhi ya maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro iliyoko Mkoani Manyara. Mpaka sasa maeneo yaliyoripotiwa kuwa na mlipuko wa ugonjwa huo ni 6, ambapo maeneo hayo ni TPC, Mabogini na Kahe kwa Mkoa wa Kilimanjaro na Msitu wa Tembo na Chemchemi kwa Mkoa wa Manyara.
Kaimu Afisa Afya wa Wilaya ya Mwanga, Ndg. Happynus Pilula amesema, japokuwa ugonjwa huo haujatokea Wilayani Mwanga, Wananchi hususani wananchi wanaoishi pembezoni mwa mto Pangani na maeneo ya bwawa la Nyuma ya Mungu, wanapaswa kuchukua tahadhari mapema ili wasipatwe na ugonjwa huo.
Ndg. Pilula amesema, mpaka sasa Wilaya imeshachukua jitihada mbalimbali ili kuhakikisha tahadhari ya mapema, inachukuliwa dhidi ya mlipuko wa ugonjwa huo. Jitihada zilizochukuliwa mpaka sasa ni pamoja na, kutoa elimu kwa wananchi, wauzaji wa vyakula na maji kuhakikisha wanafuata taratibu za afya, kusisitiza wananchi kuchemsha maji ya kunywa na kila mwananchi ahakikishe ana choo na kitumike. Jitihada zingine zilizofanywa ni, Idara ya afya imesha agiza dawa za dharura na zipo tayari ili kuhakikisha kuwa, endapo mlipuko utatokea, wananchi wanapata matibabu ya haraka.
Hata hivyo Kamati ya Halmashauri ya kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu, imeweza kuketi, na kuweka mikakati madhubuti itakayowezesha kabiliana na hali yoyote itakayopelekea mlipuko wa ugonjwa huo.
Sambamba na hilo, wananchi wote wanasisitizwa, kutoa taarifa mara moja pale wanapohisi uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo yao na kuhakikisha kuwa, wanawapeleka wagonjwa kwenye vituo vya afya mara tu wanapoona dalili za ugonjwa huo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa