Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga leo tarehe 26 Januari, 2022 kwa kauli moja, wamepitisha mpango wa bajeti ya Halmashauri kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 31.3 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Akizungumza kwenye mkutano wa Baraza hilo Mhe. Salehe R. Mkwizu ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri amesema, bajeti hii inakwenda kuakisi maendeleo ya Halmashauri pamoja na wananchi wa Mwanga.
Mhe. Mwenyekiti amesema kuwa, bajeti hii vipaumbele vyake vikuu ni pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kama kushughulikia stahiki za watumishi na kuongeza vitendea kazi, kuboresha na kuimarisha miundombinu ya mifugo na uvuvi, kusimamia utekelezaji wa sheria ya mipango miji na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kama vifaa tiba, kupunguza vifo kwa mama na mtoto, ukarabati wa miundombinu ya afya.
Vipaumbele vingine ni kuboresha miundombinu ya mifugo na uvuvi, kuongeza uzalishaji wenye tija kwa mazao ya kilimo kama korosho, katani na uboreshaji wa kilimo cha umwagiliaji, ununuzi wa zana za kilimo, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kuboresha kanzidata ya walipa kodi na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi kwa kudhibiti utoro na mimba.
Ameendelea kusema kuwa, bajeti imezingatia mambo mbalimbali kama utekelezaji wa ilani ya chama tawala, miongozo ya Serikali ikiwamo mpango wa maendeleo endelevu 2030, Dira ya Taifa 2025, kukuza fursa za ajira na uboreshaji wa miundombinu, kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na ununuzi wa samani kwa ajili ya majengo ya utawala na viongozi wa Halmashauri, kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Sambamba na hotuba yake hiyo, Mwenyekiti amesema kuwa, bajeti inayokwenda kuisha ya mwaka 2020/2021 ilikuwa na changamoto mbalimbali kama ushiriki mdogo wa wananchi kwenye kutekeleza miradi ya maendeleo, fedha za miradi kutotolewa ama kutolewa kidogo tofauti na malengo, uwezo mdogo wa Halmashauri kuchangia miradi mingi ya maendeleo, kutopatikana kwa wakati vifaa vinavyohitajika vinavyotoka kiwandani hivyo kusababisha ucheleweshaji wa baadhi ya hatua za miradi, upungufu wa watumishi katika idara mbalimbali.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa