Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Mhe. Salehe R. Mkwizu leo ameongoza Baraza lake la Madiwani la Halmashauri kujadili na kupitisha bajeti ya TARURA ya mwaka wa fedha 2022/2023. Bajeti hiyo ambayo ilisomwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Mwanga Eng. Emmanuel Festo Yohana imewafurahisha Waheshimiwa Madiwani wa Mwanga kwa kusema kuwa, bajeti hii si kwamba ni nzuri tu bali inakwenda kutatua kero ya barabara katika jamii ya wanamwanga haswa maeneo ya vijijini.
Katika hotuba yake mbele ya Waheshimiwa Madiwani, Mhe. Salehe R. Mkwizu ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, hakuacha kuweka wazi namna Serikali ya awamu ya sita inavyofanya kazi kwa kumpongeza Mhe. Rais wa Tanzani Samia Suluhu Hassan. Amesema kuwa, anatoa pongezi zake za dhati kwa Mhe. Rais kwa kuweza kuona kuwa, Waheshimiwa Madiwani ni nguzo muhimu katika kujadili na kupitisha bajeti ya TARURA na kusema kuwa, shukrani hizi haziishii hapa tu, bali anamshukuru Mhe. Rais kwa kuweza kuongeza bajeti ya TARURA Wilaya ya Mwanga kufikia kiasi cha Tsh. Bilioni 3.6.
Bajeti ya Bilioni 3.6 imelenga kufanya shughuli mbalimbali kama matengenezo ya kawaida Km 83.19 Tsh. Milioni 124.7, matengenezo ya sehemu korofi Km 95.27 Tsh. Milioni 476.7, matengenezo ya muda maalum Km 15.41 Tsh. Milioni 338.9, makalvati 14 na daraja 1 Tsh. Milioni 118.2, usimamizi na ufuatiliaji Tsh. Milioni 45.6 na fedha za utafiti Tsh. Milioni 5. Aidha TARURA imeomba kiasi cha Tsh. Milioni 985 kutoka kwenye mfuko wa maendeleo na kiasi cha Tsh. Milioni 500 fedha za majimbo ili ziweze kupelekwa kwenye kutengeneza barabara za lami na zisizo za lami.
Wakati huohuo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe, ameshukuru uongozi wa TARURA Wilaya ya Mwanga kwa kuweza kusimamia vyema katika kuchangia ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri. Amesema kuwa, TARURA wamekuwa karibu sana na Halmashauri na hii imepelekea wakandarasi wanaopata kazi hapa Wilayani kulipa ushuru na kuweza kuisaidia Halmashauri kukuza mapato ya ndani.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa