Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Abdallah Mwaipaya, leo amezindua rasmi miongozo ya elimu kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga. Miongozo hiyo ambayo ilitolewa na Ofisi ya Rais TAMISSEMI, kwa ajili ya shule za Msingi na Sekondari, imezinduliwa kwa lengo la kuwawezesha wasimamizi wa masuala ya elimu na wadau wa elimu, kufahamu maudhui yaliyo katika miongozo hiyo kwa lengo la kuendelea kuinua taaluma ya wanafunzi katika nchi yetu.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa miongozo hiyo, Mhe. Mwaipaya amesema kwamba, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, imetoa miongozo mitatu ambayo ni Mwongozo wa Uteuzi, Mwongozo wa Changamoto za Elimu na Mwongozo wa Mikakati ya Kutoa Elimu Bora katika Shule za Msingi.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Mwaipaya amesema, miongozo hii, inakwenda kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya elimu, kwani imejikita katika kuhakikisha kuwa, sekta inakuwa na viongozi bora wenye uadilifu, weledi utendaji na usimamizi mzuri.
Sambamba na hayo, Mheshimiwa Mwaipaya amesisitiza kuwa, miongozo hii inakwenda kusaidia utoaji bora wa elimu kwa wanafunzi wote wa sekondari na msingi, ikiwa ni pamoja na utatuzi wa changamoto kwa baadhi ya wanafunzi kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa wakati, kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata chakula cha mchana shuleni, pamoja na uwepo wa miundo mbinu bora, wezeshi na rafiki kwa walimu na wanafunzi.
Aidha miongozo hii itawezesha uwepo wa ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi shuleni, itahakikisha kuwa wanafunzi wanaojiunga na darasa la kwanza wanakuwa wamepata elimu ya awali, pia itasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopenda kusoma masomo ya sayansi na michepuo ya sayansi katika shule za sekondari, alisema Mheshimiwa Mwaipaya.
Kwa upande mwingine, Mheshimwa Mwaipaya amewataka wadau wa elimu pamoja na wazazi wa wilaya ya Mwanga kuhakikisha kuwa, wanashirikiana kwa karibu na walimu wanaofundisha watoto wao ili kuweza kutekeleza miongozo hii kwa urahisi, ikiwa na pamoja na kuhakikisha kuwa wanatoa ushirikiano, katika utoaji wa chakula kwa ajili ya wanafunzi na uwepo wa michezo. “Naamini tukitoa chakula shuleni, hata utoro wa wanafunzi utakuwa haupo, hii ni pamoja na kuhakikisha michezo inakuwepo shuleni ili kupunguza utoro”, alisema Mheshimiwa Mwaipaya.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe, amesema kuwa, wadau wa elimu na wazazi, ni miongoni mwa watu muhimu sana katika Wilaya ya Mwanga, kwani wanao uwezo mkubwa wa kusaidia walimu na wanafunzi kuwa na mazingira bora ya kusomea na kujifunzia. Amewaasa na kuwaomba wadau wa elimu na wazazi kuhakikisha kuwa, wanaunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na utoro shuleni, uwepo wa chakula cha mchana na uwepo wa makazi bora ya walimu.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa