Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe leo amekutana na watumishi wa idara mbalimbali kutoka kwenye ngazi ya Kata. Watumishi aliokutana nao ni Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji, Wataalamu wa Afya, Maafisa Mifugo, Maafisa Kilimo, Waratibu Elimu Kata, Wakuu wa shule na Walimu Wakuu.
Mkurugenzi amekutana na watumishi hao katika ukumbi wa Mwanga Sekondari ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku na kupata wasaa wa kuwakumbusha na kuwaelekeza juu ya masuala mbalimbali ya utendaji kazi za Serikali za kila siku.
Akiwa katika kuwakumbusha na kuwaelekeza juu ya majukumu yao, Mkurugenzi amesema kuwa, watumishi wa umma wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia mambo makuu matatu ambayo ni Sera, Taratibu na Kanuni (STK). Amewakumbusha kuwa, vyeo walivyonavyo ni dhamana hivyo wanapaswa kuvifanyia kazi kwa usahihi kwa manufaa ya serikali na wananchi wake na siyo kwa maslahi binafsi. “Mkae mkijua kuwa, vyeo mlivyonavyo siyo kwamba nyie ni bora kuliko wengine, bali hicho cheo ni dhamana, na wala usiwanyanyase unaowaongoza, bali waelekeze”, alisema Mkurugenzi.
Aidha katika maelekezo yake, hakuacha kuzungumzia suala la watendaji wa serikali kutoka ofisini na kwenda kwa wananchi na kutatua kero zinazo ikabili jamii. Amewataka watumishi hao kuhakikisha kuwa, wanafanya kazi kwa uwadilifu na uwajibikaji. Ameendelea kusema kuwa, baadhi ya watendaji wa vijiji wamekuwa kama miungu watu, hawataki kutembelea wananchi na kuatatua kero zao. Amesisitiza kuwa, haipendezi kuona mambo madogo yanayoweza kutatuliwa katika ngazi za chini yanafika ofisini kwake ama kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Masuala kama hayo yatatuliwe katika ngazi za chini na yakishindikana kabisa, ndipo yafike katika ngazi za juu, amesema Mkurugenzi.
Sambamba na hayo, pia hakuacha kuzungumzia kukerwa na baadhi ya watendaji wa serikali kuzembea suala la ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri. Amesema kuwa, kuna baadhi ya watumishi wa Halmashauri wamepewa kazi ya kusimamia na kukusanya mapato ya Serikali lakini hawafanyi kazi hiyo kwa ufasaha hata wakati mwingine wanafikia hatua ya kuhujumu juhudi za ukusanyaji wa mapato. Mkurugenzi amesema kwamba, watumishi wa namna hii hata wanyamazia na atawachukulia hatua za kinidhamu pale atakapobaini kuna uzembe katika suala la kukusanya mapato ya Serikali.
Akizungumza juu ya miradi mbalimbali ya Serikali amesema kuwa, kuanzia sasa ameamua vifaa vyote vya ujenzi vitakavyohitajika kwa ajili ya kujenga miradi inayoendelea hapa Wilayani, vitaagizwa kiwandani na vifaa vichache ambavyo vitakuwa havipatikani kiwandani vitaagizwa kutoka kwenye maduka ya kawaida. Lengo kuu likiwa ni kuokoa gharama kubwa zinazotumika katika kununua vifaa vya ujenzi kutoka kwenye maduka ya kawaida. Amesisitiza kuwa, vifaa kama saruji, chokaa, mabati, nondo, mbao na rangi vitakuwa vinaagizwa kutoka kiwandani ili kuokoa gharama za ujenzi.
Katika mazungumzo yake, Mkurugenzi amewasisitiza watumishi wote wa Halmashauri ya Mwanga kuhakikisha kuwa wanachanjwa chanjo ya UVIKO – 19. Amesema kuwa, watumishi wamepewa dhamana ya kuaminiwa na serikali na ndiyo maana wao ni watumishi wa umma, hivyo wanapaswa kuwa mfano bora katika kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanikiwa kwa wao kuchanjwa na kuihamasisha jamii nayo ili iweze kupata chanjo. “Chanjo hii ni salama, na ndio maana mimi Mkurugenzi wenu pamoja na DC wenu tumechanja na hatujapata madhara yeyote, hivyo kila mtumishi ahakikishe anapata chanjo hii kwa ajili ya afya yake na jamii yake”, Amesema Mkurugenzi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa