Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga imeahidiwa kupatiwa kiasi cha Tsh. Milioni mia tano kutoka Serikalini kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya. Ahadi hiyo ilitolewa na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) alipofanya ziara yake Wilayani Mwanga tarehe 17 Novemba, 2021 na kukutana na Baraza la Madiwani pamoja na Wajumbe wa CMT. Mhe. Mwalimu alisema kwamba, kiasi hicho cha fedha kitaletwa katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha wa serikali, yaani 2021/2022.
Sambamba na hayo, Mhe. Waziri amesema kwamba, Kata ya Kivisini itapatiwa kiasi cha Tsh. Milioni 600, fedha ambazo zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Kata hiyo. Kata ya Kivisini ni kata ambayo haina sekondari, hivyo ujenzi wa shule hii utasaidia wanafunzi wengi wanaofaulu kuingia kidato cha kwanza kupata fursa ya kuendelea na masomo, hususani wanafunzi wanaotoka kata ya Kivisini na kata za jirani.
Aidha, Mhe. Waziri ametoa maelekezo na kuagiza uongozi wa Wilaya kuhakikisha kuwa, fedha za tozo zilizoletwa Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kiasi cha Tsh. Milioni 250 zipelekwe katika kata ya Kirya kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya cha afya cha kata hiyo. Kata ya kirya ni miongoni mwa kata ambazo zina wakazi wengi hivyo kituo hiki cha afya kitakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wakazi wa kata hii pamoja na maeneo ya kata za jirani. Pia kituo hiki kitasaidia kutoa huduma kwa wakazi wa Wilaya jirani ya Simanjiro kutokana na ukaribu na muingiliano uliopo.
Katika ziara yake hiyo, hakuacha kutoa pongezi kwa uongozi wa Wilaya kwa kufanya kazi vizuri na kwa bidii. Amesema kuwa, ameridhishwa na utendaji kazi mzuri na ushirikiano uliopo kati ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Baraza la Waheshimiwa Madiwani na timu ya wataalamu wa Halmashauri. Ameendelea kusema kwamba, anaridhishwa na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayoendelea hapa Wilayani miongoni mwayo ikiwa ni ile iliyoletewa fedha za UVIKO 19.
Katika kikao chake na Waheshimiwa madiwani, Mhe. Waziri amesema, “Natambua kuwa kila Diwani anahitaji apate fedha za maendeleo ya kata yake, lakini mimi nawashauri, ni bora miradi itekelezwe michache, ambayo itakamilika kwa wakati kuliko kugusa kidogokidogo kwa kila kata na isikamilike”. Utekelezaji wa miradi mingi kwa wakati mmoja inapelekea miradi mingi kukwama kwasababu fedha ni kidogo na miradi inakuwa mingi, hivyo ni bora itekelezwe michache ya kuonekana na yenye kukamilika, Alisema Mhe. Waziri. Amewaomba Madiwani kuhakikisha kuwa, fedha za miradi ya maendeleo ambayo ni asilimia 40 ya makusanyo ya mapato ya ndani, wahakikishe wanazisimimia vizuri na ziende kwenye miradi kama utaratibu unavyoelekeza.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa