HONGERA AFISA ELIMU MSINGI KWA KUWAJALI WALEMAVU
Ni jambo la kufurahisha pale unapompata mtu mwenye roho ya huruma tena ya kuwajali wenye mahitaji maalumu kama watoto walemavu kwani watoto wenye mahitaji maalum wanahitaji kufarijiwa, kutunzwa na kuthaminiwa.
Hongera hizi zinaenda kwa Afisa Elimu Msingi Ndugu Allan S. Said kwani kwa mara ya kwanza anafanya kitu chenye taswira nzuri ndani ya jamii kwa kuwakutanisha kwa pamoja watoto wenye mahitaji maalum wa Shule za Msingi na kula nao chakula pamoja na kuwapatia zawadi mbalimbali.
Tukio hili ambalo liliwajumuisha watu mbalimbali pamoja na taasisi binafsi lilifanyika kwenye uwanja wa michezo wa C. D. Msuya siku ya jana tarehe 06 Machi, 2018 na kuhudhuriwa na walimu, wananchi, wazazi wa watoto wenye mahitaji maalum pamoja na taasisi mbalimbali kama Benki ya Wananchi Mwanga, Benki ya NMB na taasisi ya Tanesco.
Akizungumza kwa moyo uliojawa na furaha huku machozi yakimlengalenga kwa namna alivyofurahia jambo hilo Mhe. Theresia P. Msuya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ambaye pia alikuwa mgeni rasmi alimpongeza sana Afisa Elimu kwa jambo nzuri alilolifanikisha kwa kuwajali watoto hao ambao wanasoma shule zenye mahitaji maalum. Mwenyekiti wa Halmashauri aliendelea kutoa pongezi kwa wote waliotoa michango yao kwa kuhakikisha kuwa watoto hao wanafurahi na kujisikia kuwa nao ni sehemu ya watu wengine. Taasisi zilizotoa michango na zawadi na kuhakikisha kuwa tukio hilo linakwenda vizuri ni pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi, Idara ya Elimu Msingi, Hawa Fashion, Benki ya NMB, Benki ya Wananchi Mwanga, Shirika la Umeme Tanesco Mwanga, Walimu wa shule za Mwanga na watu binafsi.
Akizungumzia juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wenye ulemavu Mhe. Mwenyekiti alisisitiza kuwa kwa sasa ameona kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa shule zenye watoto wenye mahitaji maalum kuwa na walimu wa kutosha na atahakikisha suala hili analisemea kwenye vikao vya Halmashauri ili walimu waliopo kwenye shule hizo wasije wakahamishwa kwani hata hao waliopo hawatoshi kulingana na umuhimu wa watoto hao japokuwa inaonekana kama walimu waliopo kwenye shule za watoto wenye ulemavu ni wengi.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri Ndg. Golden A. Mgonzo akizungumza mbele ya watoto hao alisisitiza kuwa watoto wote wanapaswa kupata malezi mazuri pasipo kujali hali zao na ofisi yake iko makini kuhakikisha yeyote atakaye husika katika kuwanyanyasa watoto ndani ya Wilaya yake watapitiwa na mkono wa sheria. Pia aliwaasa wazazi wa watoto wote kuhakikisha kuwa wanafuatilia haki za watoto wao kwenye Ofisi za Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii pale wanapopatwa na matatizo ambayo hawawezi kuyakabili.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa