Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndg. Tixon T. Nzunda, jana alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga.
Katika ziara yake hiyo, Ndg. Nzunda alieleza kufurahishwa na suala nzima la usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kwa kusema kwamba, miradi ya maendeleo ya Halmashauri inajengwa vizuri na kwa viwango vinavyo stahili.
Akiongea wakati wa kukagua miradi na kwenye kikao cha majumuisho ambacho kilijumuisha Kamati ya Usalama Wilaya, Maafisa Tarafa, Wakuu wa Divisheni na Watendaji wa Kata, alisema; “Natoa pongezi za dhati kwa uongozi wote wa Wilaya na watendaji wake kuanzia Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji, Wakuu wa Divisheni, Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi ya maendeleo kwa manufaa ya Watanzania”.
Aidha Katibu Tawala Mkoa amewataka Wakuu wa Divisheni kuhakikisha kuwa, wanaendelea kusimamia miradi yao kwa karibu ili ikamilike kwa wakati, na ianze kutumika. Amewahimiza kuhakikisha kuwa, wanampa Mkurugenzi Mtendaji ushirikiano wa hali na mali ili malengo ya Serikali yaweze kutimizwa kwa wakati.
Wakati huohuo, Katibu Tawala, amewahimiza watendaji na viongozi wa serikali kuhakikisha kuwa, wanafanya kazi za Serikali kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu kwa mujibu wa miongozo ya utumishi wa Umma. Amewataka watumishi wa Serikali kuhakikisha kuwa, kero na malalamiko ya wananchi yanafanyiwa kazi kwa wakati pasipo ubaguzi wa rangi wala jinsia. “Watumishi mnapaswa kufahamu kwamba, bosi wenu wa kwanza ni mwananchi, hivyo mnapaswa kuwathamini, kuwajali na kuwapatia huduma kwa wakati pale wanapofika ofisini kwenu, Alisema Katibu Tawala”.
Katibu Tawala, alifanya ziara yake Wilayani Mwanga jana tarehe 15.08.2023 ikiwa ni sehemu ya majukumu yake ya kawaida kwa kuhakikisha kuwa, anasimamia shughuli za kiutendaji na utawala katika Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa