Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Ndugu Mariana Sumari, leo ametoa shukrani za dhati kwa shirika lisilokuwa la Serikali la World Vision Tanzania, kwa namna linavyofanya kazi nzuri ya kuinua elimu hapa Wilayani Mwanga.
Kaimu Mkurugenzi ametoa pongezi hizo kwenye hafla iliyofanywa na shirika hilo, ikiwa na lengo la kutoa pongezi na zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye utengenezaji wa zana za kusomea na kujifunzia (KK).
Katika kuhakikisha kuwa, shirika linaendeleza elimu Wilayani Mwanga, limeweza kutekeleza programu yake kwenye vijiji sita vya kata ya Kirya na Lembeni, ambavyo ni Kiruru, Kisangara, Mangara, Mbambua, Lembeni na Njiapanda. Mojawapo ya mafanikio ambayo shirika limeweza kufikia hususani katika elimu ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali ambao wamekuwa watekelezaji na wawezeshaji wa mradi wa kuinua elimu hapa wilayani. Walioweza kupatiwa mafunzo ni pamoja na walimu wakuu, walimu, wazazi, waratibu elimu, maafisa elimu na wanasihi. Wadau hawa wamekuwa kama nyenzo muhimu sana katika kuendeleza programu hii inayosimamiwa na shirika.
Mafanikio mengine ambayo shirika limepata katika jitihada zake za kuinua elimu ni pamoja na, kusambaza vitabu vya kujifunzia, kusambaza vifaa vya michezo, shajala na uanzishwaji wa kambi maalum zinazotumika kuwafundishia watoto kwa kila siku za jumamosi wanapokuwa hawaendi shuleni. Katika kuhakikisha kuwa watoto wanaelewa kwa urahisina kwa haraka, madarasa wanayosomea (makambi) yanapambwa na picha na michoro mbalimbali ili kumuwezesha mtoto kuelewa.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa