Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Mwanga Bi. Mariana Mgonja, leo amefanya kikao kazi na wataalamu wake ambao ni Maafisa wa Idara ya elimu msingi, Waratibu Elimu Kata na Walimu Wakuu. Kikao hicho lengo lake kuu lilikuwa ni kuona changamoto zilizopo shuleni, namna ya kuzitatua na kuweka mikakati mizuri ya kitaaluma itakayo wezesha taaluma kupanda haswa kwa madarasa yenye mitihani, ambayo ni darasa la saba na darasa la nne.
Pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo shuleni, Afisa Elimu amewaagiza walimu wakuu na waratibu elimu kata kuhakikisha kuwa, wanaishi kwenye maeneo yao ya kazi ili muda wote waweze kukabiliana na changamoto zilizopo. "Haiwezekani kituo chako cha kazi kiwe Mwanga halafu uishi Same". Amesema Afisa Elimu.
Katika kikao kazi hicho, Afisa Elimu kwa kushirikiana na Maafisa wa Idara yake, walimu wakuu na waratibu, waliweka mikakati ambayo wataisimamia kwa mwaka 2019 ili shule ziweze kufanya vizuri kwenye ufaulu. Baadhi ya mikakati iliyowekwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanakula chakula cha mchana shuleni, kuwa na mtihani mmoja unaofanana wa nusu muhula na muhula kwa shule zote, kudhibiti utoro, kuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, kutafuta walimu wa ziada na iwekwe mikakati ya namna ya kuwalipa na walimu wawe wanafundisha katika muda wa ziada.
Mikakati mingine ni kutoa motisha kwa wanafunzi na walimu wanaofanya vizuri, kumaliza silabasi kwa wakati, kuwa na michezo ili kupunguza utoro na kuifanya akili ichangamke, kuunda klabu za masomo na kuwapa wanafunzi kazi za nyumbani (home work).
Pamoja na hayo, Afisa Elimu amewaomba walimu kuonyesha ushirikiano ili kazi zifanyike kwa ufanisi mzuri. Pia amewataka wale wenye matatizo mbalimbali kama madai ya uhamisho waweze kufika ofisini kwake ili ajue anawezaje kuwasaidia katika kutatua changamoto zao. Pia amewataka walimu wakuu waendelee kushirikiana na jamii zinazo wazunguka na kuwashirikisha kwenye masuala yanayohusu shule ili waweze kuleta maendeleo ya shule zao.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa