Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, kwa kushirikiana na wataalam wa Halmashauri, jana imetembelea Bwawa la Nyumba ya Mungu kwa lengo la kubaini na kuweka mikakati mizuri ya kuweza kuinua kiwango cha makusanyo ya mapato yatokanayo na uvuvi wa samaki na mazao yatokanayo na samaki..
Kamati hiyo iliyo ongozwa na Mhe. Mwenyekiti wa Halmashauri, Bi.Theresia P. Msuya, iliweza kukutana na vikundi vinavyohusika na uangalizi na uzuiaji wa uvuvi haramu (BMU - Beach Management Unit) na kupokea changamoto mbalimbali ambazo BMU wanakutana nazo. Vikundi hivyo vilieleza kuwa, miongoni mwa changamoto walizonazo ni pamoja na kina cha maji kupungua kwa haraka kutokana na uhitaji wa maji ya umwagiliaji, nyavu kuibiwa mara kwa mara, kuonewa na vyombo vya dola, ufungaji wa bwawa mara kwa mara, ushuru mkubwa wa samaki, uwepo wa wanyama aina ya viboko ziwani na uhaba wa wataalam wa uvuvi.
Pamoja na changamoto hizo, Mhe. Theresia akiongea na wavuvi hao kwa nyakati tofauti, alisema, suala la kufunga bwawa mara kwa mara lipo mikononi mwa wavuvi wenyewe, endapo wataacha kutumia nyavu haramu na kuvua samaki wadogo, bwawa haliwezi kufungwa, ila wakitumia nyavu haramu bwawa litafungwa.
Mhe. Theresia aliendelea kusisitiza kuwa, ni jukumu la kila mvuvi kuhakikisha anazuia uvuvi haramu kwa kuachana na kutumia makokoro ili wavuvi wapate kipato na Serikali ipate kipato. Pia ameagiza kuwa, kila mwenye mtumbwi ahakikishe ameusajili kwani kuna baadhi ya mitumbwi haina nambaza usajili.
Ameongeza kuwa, Halmashauri ina fedha nyingi za kukopesha vijana, wanawake na walemavu. Hivyo anatoa wito kwa wavuvi, kujiunga kwenye vikundi vidogovidogo ili waweze kuomba mkopo na uwasaidie kwenye shughuli zao za uvuvi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ni miongoni mwa Halmashauri zilizofanya vizuri sana kwenye ukusanyaji wa mapato kwa mwaka 2017/18. Kwa mwaka 2018/19, Halmashauri imejipanga kuhakikisha kuwa, inaendelea kufanya vizuri zaidi kwenye ukusanyaji wa mapato na ndio maana kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango imefanya ziara yake kwenye chanzo hiki cha mapato yatokanayo na samaki na mazao yake, kwa lengo la kujifunza, kubaini na hatimaye kutoa ushauri kwa wataalam juu ya namna bora na nzuri ya kukusanya mapato ya Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa