Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, jana tarehe 11 Mei, 2023, ilitembelea na kukagua viwanda sita vilivyopo katika Wilaya ya Mwanga. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kujionea namna ambavyo viwanda hivyo vinafanya kazi za uzalishaji, pamoja na kujifunza teknolojia zinazotumika katika kuendesha viwanda hivyo. Viwanda vilivyo tembelewa ni Kiwanda cha kokoto Kifaru, Kiwanda cha Katani Kisangara (Mahamed Enterprises) na Kiwanda cha Shaba Kiruru (Mega Copper). Vingine ni Kiwanda cha Maji Lambo (Mwanga Pure Drinking Water), Kiwanda cha Kifaru Biochem na kiwanda cha mikate (Kifaru Bakery and Confectionery).
Wajumbe wa Kamati hiyo, walisema kwamba, wanafurahishwa na uwepo wa viwanda vingi hapa Wilayani Mwanga, kwani vimekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi haswa vijana. Akiongea kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira Mhe. Innocent J. Msemo alisema kwamba, uwepo wa viwanda hapa wilayani, ni fursa nzuri kwa kutoa ajira, kukuwa kwa uchumi wa Mwanga na Taifa, pamoja na kuchochea maendeleo ya wazawa.
Aidha, Kamati hiyo, iliwaasa wamiliki wa viwanda Wilayani Mwanga kuhakikisha kwamba wanatunza mazingira vizuri ili kuepuka uchafuzi wa mazingira. Pia wamesisitizwa kuendelea kuongeza fursa za ajira haswa kwa wazawa.
Uwepo wa viwanda Wilayani Mwanga imekuwa ni chachu kubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Viwanda vingi vimekuwa vikisaidia kuunga mkono ujenzi wa barabara, kuchangia ujenzi wa miundombinu ya Elimu, kutoa maeneo ya kilimo cha muda kwenye mashamba, ajira za muda mfupi na muda mrefu, mafunzo ya ujasiriamali, kujenga viwanja vya michezo na kutoa vifaa vya kujifunzia shuleni kama computer.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa