Kikundi cha Sanaa na Utamaduni cha Mwanga kinacho fahamika kwa jina la "Teule Cultural Group", ambacho kiliwakilisha Mkoa wa Kilimanjaro kwenye Tamasha la Kitaifa la Utamaduni, kwa mara ya pili mfululizo kimeshika nafasi ya kwanza Kitaifa kwenye mashindano yaTamasha la Utamaduni lililo andaliwa na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Kikundi hicho ambacho kinatokea Kata ya Kifula Wilayani Mwanga, kimeshika nafasi ya kwanza kwenye kipengele cha Vyakula vya Asili.
Tamasha hilo ambalo limefanyika Mkoani Njombe kwa kuhusisha mikoa ya Tanzania Bara, lilianza tarehe 25.08.2023 na kuhitimishwa leo tarehe 27.08.2023.
Kikundi cha Teule Cultural Group kilishiriki katika Tamasha hilo kwa kuuwakilisha Mkoa wa Kilimanjaro kwa vipengele vya ngoma za asili na vyakula vya asili.
Kikundi kiliweza kucheza ngoma ya mjungu, ngoma ambayo huchezwa na jamii ya Wapare wa Wilaya ya Mwanga na katika upande wa vyakula vya asili, kikundi kiliweza kupika vyakula mbalimbali vya asili ambavyo vinaliwa na makabila yaliyopo Mkoani Kilimanjaro kama makande, kishumba, kirembwe, viazi vikuu, pombe za asili kama dengelua, mbege, nk.
Tamasha hilo ambalo limehitimishwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum) Mhe. George H. Mkuchika, ni tamasha ambalo limefanyika mwaka wa pili mfululizo na linategemewa kufanyika mwaka 2024 Mkoani Morogoro.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa