Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Abdallah Mwaipaya, amezitaka taasisi na mashirika mbalimbali yasiyo ya Serikali na yanayo fanya kazi Wilayani Mwanga kuhakikisha kwamba, wanafuata maadili ya Mtanzania pale wanapokuwa katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo jana alipokutana na taasisi pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya shughuli zake Wilayani Mwanga. Akitoa hotuba yake mbele ya wawakilishi wa mashirika hayo, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alisisitiza kwamba, kumekuwepo na tabia kwa baadhi ya NGO na CBO kufanya kazi zake hapa Wilayani pasipo kuzingatia maadili ya Mtanzania na kupelekea kuingiza tamaduni zilizo kinyume na tamaduni halisi za Mtanzania.
Aidha Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alisisitiza kwamba, mashirika yote yanayofanya kazi Wilayani Mwanga, lazima yazingatie maadili ya Mtanzania. Pia alisisitiza kwamba, mashirika hayo yatoe ushirikiano wa karibu kwa Serikali na kuhakikisha kwamba, taarifa mbalimbali zinazo hitajika na kutoka kwao zinatolewa kwa wakati uliokusudiwa.
Sambamba na hayo, Mkuu wa Wilaya alitoa rai kwa NGO hizo kuhakikisha kuwa, taarifa za miradi inayo tekelezwa na mashirika hayo, zinawafikia wananchi wa maeneo ambayo mradi unatekelezwa, kwani kwa kufanya hivyo italeta tija kwa ustawi wa mashirika hayo pamoja na jamii husika.
Pamoja na hayo, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, alisisitiza wamiliki wa mashirika hayo kufanya kazi kwa karibu na ofisi yake ikiwa ni pamoja na kuwasilisha ofisini kwake changamoto mbalimbali ambazo mashirika hayo yamekuwa yakikabiliana nazo ili kuangalia namna bora na nzuri ya kutatua changamoto hizo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa