Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, leo imezindua rasmi kituo cha afya Kirya na huduma zote za wagonjwa wa nje zimeanza kutolewa. Kituo hicho ambacho kinategemewa kutoa huduma kwa wananchi wa Kirya wapatao 8554, na wananchi wa Wilaya jirani za Same na Simanjiro ya Mkoa wa Manyara, kimekamilika kwa wakati muafaka kutokana na wananchi wa Kata ya Kirya hapo awali kupata huduma hiyo kwenye maeneo yaliyopo zaidi ya kilomita 25.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Ndg. Abdallah Mwaipaya, ambaye amekifungua kituo hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, alisema, kituo hiki ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Mwanga hususani wananchi wa Kata ya Kirya na maeneo ya jirani. Amewataka wananchi hao kuhakikisha kwamba, wanakilinda na kukitunza kituo hicho ili wafaidi huduma ambazo zitakuwa zikitolewa hapo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Mhe. Salehe R. Mkwizu amesema kwamba, baada ya kituo hiki kukamilika, Baraza la Madiwani kwa pamoja waliridhia kutoa kiasi cha Tsh. Milioni 10 kupitia mapato ya ndani ili ziweze kununua vifaa tiba na madawa, na huduma ziweze kuanza kutolewa kituoni hapo. "Nawapongeza Waheshimiwa Madiwani wangu kwa kukubali kiasi cha Tsh. Milioni 10 za mapato ya ndani zitolewe na ziweze kutumika kununulia madawa na vifaa tiba kwa ajili ya wananchi wa Kirya", alisema Mhe. Mkwizu.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilileta kiasi cha Tsh. Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za nje (OPD) na Maabara. Fedha hizo, ndizo zilizotumika kukamilisha majengo hayo na huduma kuanza. Aidha, kiasi kingine cha Tsh. Milioni 250 kimeletwa tena na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji, na huduma ya Mama na Mtoto.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa