Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Abdallah Mwaipaya, jana amepokea madawati 236 kutoka benki ya Mwanga Hakika. Madawati hayo yametolewa na benki hiyo ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika sekta ya elimu ndani ya wilaya ya Mwanga.
Mhe. Mkuu wa Wilaya ameushukuru uongozi wa benki ya Mwanga Hakika kwa kuonyesha mwitikio chanya katika kuendeleza sekta ya elimu hapa wilayani Mwanga. Ameuomba uongozi huo kuendelea kutoa ushirikiano kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo kwani kwa kufanya hivyo wataifanya Mwanga ikue haraka zaidi kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa benki hiyo wakati wa kukabidhi madawati hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Mwanga Hakika Eng. Ridhiwani Mringo alisema, wameamua kutoa madawati hayo kwa ajili ya shule za sekondari ili kuonyesha ni kwa namna gani benki hiyo inatoa mchango wake kwa jamii hususani kwa jamii ya Mwanga.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe ametoa shukrani zake kwa benki hiyo kwa kusema, kabla ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza 2022, Halmashauri ilikuwa na upungufu wa madawati 689, lakini mpaka sasa changamoto hiyo haipo kabisa. Alisema kuwa mpaka sasa Halmashauri ya Mwanga imetengeneza madawati 400, benki ya NMB watatoa madawati 200 na benki ya CRDB nao watachangia madawati 16 na kufanya pawepo na zidio la madawati zaidi ya 100.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa