Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, leo imeweza kumuenzi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassani, kwa vitendo baada ya Waheshimiwa Madiwani na Timu ya Wataalamu wa Halmashauri kufanikiwa kufanya ziara ya kitalii katika, hifadhi ya mbuga za wanyama ya Mkomazi iliyopo Mkoa wa Kilimanjaro.
Ziara hiyo, ambayo ilikuwa na lengo la kumuunga mkono Rais Samia, katika kuutangaza utalii wa Tanzania kupitia Royal Tour, pamoja na kutoa fursa ya kujifunza kwa ajili ya kuboresha sekta ya utalii Wilayani Mwanga, imekuwa ya manufaa makubwa kwa washiriki, kwani wamejifunza mengi ikiwa ni pamoja na kupata elimu ya uhifadhi, namna ya kutangaza vivutio vya kitalii na kuviendeleza kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vya baadae.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Bi. Mwajuma A. Nasombe, akizungumza wakati wa ziara hiyo amesema, ziara hii ya utalii wa ndani, imelenga kumuunga mkono kwa vitendo Rais Samia, kwa kuutangaza utalii wa nchi yetu ya Tanzani. Amesisitiza kwamba, pamoja na kumuunga mkono Rais, Halmashauri yake imejifunza mengi ikiwa ni pamoja na kwenda kuanza mikakati ya kuhakikisha kwamba, anazishirikisha mamlaka za uhifadhi wa mbuga hiyo, ili waweze kuanzisha lango la watalii katika kijiji cha Kwakoa Wilayani Mwanga. Ameendelea kusema kwamba, pamoja na kujifunza mengi, ziara hiyo ya utalii wa ndani imekuwa sehemu ya kufurahi pamoja na kupunguza msongo wa mawazo kwani, waheshimiwa madiwani na watumishi, wamekuwa wakifanya kazi muda mrefu, hivyo ziara kama hizi zinapunguza msongo wa mawazo ikiwa ni pamoja na kuchangamsha mwili na akili.
Tangu Rais Samia azindue filamu ya "Royal Tour", sekta ya utalii nchini, imeendelea kukuwa kwa kasi, kutokana na muitikio mkubwa wa ujio wa watalii, kutoka nje ya nchi, pamoja na uwepo wa watalii wengi wa ndani ambao wamekuwa wakitembelea maeneo mbalimbali, yenye vivutio vya kitalii.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa