Mbunge wa Mwanga Mhe. Joseph Anania Tadayo ameeleza kuwa, Ziwa Jipe ni chanzo kikubwa cha maendeleo ya uchumi wa wanamwanga ikiwa ni pamoja na kuchangia kwa asilimia kubwa katika kuendeleza miradi mikubwa ya Serikali.
Mhe. Mbunge aliyasema hayo wakati akiwa kwenye ziara maalum iliyofanywa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Hamad Hassan Chande tarehe 20 Septemba, 2021. “Ziwa Jipe ni ziwa linalotegemewa kama chanzo moja wapo muhimu cha kupeleka maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, bwawa ambalo linatumika kuzalisha umeme, pia bwawa hili ni sehemu ya chanzo cha mradi mkubwa wa maji wa Mwanga – Same – Korogwe” alisema Mhe. Tadayo. Kutokana na umuhimu wa Ziwa hili katika miradi hii mikubwa ya Taifa, ni vyema serikali ikaweka nguvu katika kutatua changamoto ya magugu maji yaliyopo katika Ziwa Jipe, aliendelea kusema Mhe. Tadayo.
Aidha, Mhe. Mbunge akiendelea kuelezea umuhimu wa ziwa jipe, alisema, ziwa hili ni chanzo cha uchumi kwa wananchi wa Mwanga. Ziwa linapopeleka maji katika bwawa la Nyumba ya Mungu, wanachi wa bwawa hilo nao wananafaidika kwa kufanya shughuli za uvuvi na kuwa sehemu ya kichocheo cha maendeleo ya uchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Ziwa Jipe lenye ukubwa wa kilomita za mraba 30 linakabiliwa na magugu maji kwa asilimia kubwa, magugu ambayo yanahatarisha ziwa hilo kupotea ama kupungua ukubwa wake hususani upande wa Tanzania.
Katika kuhakikisha kuwa changamoto ya magugu maji yanatafutiwa njia ya kuyaondoa, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira alisema, Serikali imesha andaa andiko maalum kwa ajili ya kutafuta fedha za kuondoa magugu maji hayo. Alisisitiza kuwa, wakati serikali ikiendelea kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili, jitahada za makusudi zitaendelea kuchukuliwa na Serikali ili kuendelea kukabiliana na changamoto ya magugu maji hayo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa