Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Anna Mghwira, leo amefanya kikao na Wakurugenzi wa Halmashauri na wadau wa maendeleo lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa, panakuwepo na mikakati thabiti ya kuwekeza Mkoani hapa, kwa kuzitumia fursa za uwekezaji zilizopo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema, kuanzia sasa Mkoa utahakikisha unasimamia na kuanza kutafuta wawekezaji ama wadau watakao jenga uwanja wa mpira wa King George Memorial na ujenzi wa soko la Kimataifa la nafaka la Lokolova litakalo jengwa Himo.
Aidha wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Kilimanjaro waishio Dar es Salaam (KDF), waliwasilisha ramani ya mfano kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa wa namna ambavyo uwanja wa King George Memorial utakavyokuwa. Wadau hao wamesema, uwekezaji huo mkubwa utakuwa na manufaa makubwa kwa watu mbalimbali. Wamesema mbali na uwepo wa viwanja vya michezo, pia patakuwepo na huduma mbalimbali kama, maeneo ya biashara, hospitali ya kisasa na sehemu mbalimbali za burudani. Wadau hao pia waliwasilisha ramani ya mfano ya namna ambavyo, soko la kimataifa la nafaka, Lokolova litakavyokuwa.
Katika kuhakikisha kuwa jambo hili linafanyika kwa haraka, zimeundwa kamati tatu ambapo kila kamati imepewa jukumu lake. Kamati ya kwanza imepewa jukumu la kufuatilia na kuhakikisha wafanyabiashara wa soko la Memorial wanatafutiwa eneo lingine la biashara, kamati ya pili imepewa jukumu la kufuatilia hati miliki ya ardhi litakapo jengwa soko la nafaka la kimataifa la Lokolova na kamati ya tatu imepewa jukumu la kuhakikisha, inafuatilia vitega uchumi ama fursa za utalii zilizopo mkoani Kilimanjaro na kufuatilia eneo ambalo linaweza kufaa kwa ajili ya viwanda vya kisasa.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amesema, sasa hivi ni muda muafaka wa Mkoa kuhakikisha unaendelea kwa kutumia fursa za uwekezaji, zilizopo takribani Wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro, hivyo kila kamati iliyopewa majukumu, ihakikishe inasimamia vizuri majukumu yake na kutoa taarifa kwa wakati.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa