Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, jana alifanya ziara yake ya kikazi Wilayani Mwanga na kuweza kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji ambapo ni mradi mkubwa wa Kitaifa unaogharimu takribani shilingi bilioni 336. Mradi huu unategemewa kuwanufaisha wananchi wa wilaya tatu za Mwanga, Same na Korogwe.
Akiwa anawahutubia wananchi wa Mwanga, Mhe. Makamu wa Rais, aliwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Mwanga kwa kuendelea kutunza na kudumisha amani kwenye wilaya. Alisema kuwa, amani ni jambo la msingi na inapaswa kudumishwa na kutunzwa kwani pasipo amani, hata maendeleo hayatakuwepo. Pia aliwapongeza wananchi kwa kuendelea kuzalisha chakula na kuhakikisha wanapata chakula cha kutosha kwa ajili ya kuendesha maisha yao ya kila siku.
Mhe. Makamu wa Rais pia hakuacha kukemea tabia ya baadhi ya viongozi wa nchi kuacha kuzingatia uongozi na utawala bora. Alisema kuwa, viongozi wa nchi wasiposhirikiana kwenye utendaji pale wanapokuwa kwenye maeneo yao ya kazi, hapatakuwepo na maendeleo. Pia hakuacha kuwaomba wanachi kuhakikisha kuwa, mwaka 2019 ambao utakuwa mwaka wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, kuchagua viongozi wazuri, wepesi na wenye uchu wa maendeleo kwa wanachi wa Mwanga.
Akizungumzia suala la upungufu wa walimu shuleni, Mhe Makamu wa Rais alisema, Serikali inalitambua hilo na itajitahidi kuhakikisha inapunguza tatizo la upungufu wa zaidi ya walimu 300 ambapo ni upungufu mkubwa. Sambamba na hilo amewasisitiza viongozi wa Halmashauri kuendelea kukusanya mapato kwa bidii kubwa ili kuendelea kumalizia miradi midogo kama zahanati na vituo vya afya. Alisema, serikali kuu ina miradi mingi na mikubwa inayo iendesha, hivyo halmashauri wahakikishe miradi midogo wanaimalizia na kuiendeleza.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa