Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Abdallah Mwaipaya, leo amezindua zoezi la kuvalisha hereni mifugo ya wafugaji Wilayani Mwanga. Uzinduzi wa zoezi hilo umefanyika katika Kijiji cha Kwakihindi Kata ya Kigonigoni na kushuhudiwa na jamii ya wafugaji wa kimasai pamoja na viongozi wa wafugaji wa wilaya ya Mwanga.
Katika uzinduzi huo Mhe. Mkuu wa Wilaya amewaasa wafugaji wote wa Wilaya ya Mwanga kuhakikisha kuwa mifugo yao inavalishwa hereni kwa mujibu wa sheria. “Zoezi hili siyo la kwangu wala siyo la Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, bali ni zoezi ambalo lipo kisheria na Serikali inalitambua kwa mujibu wa sheria ya utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo ya mwaka 2010”, alisema Mkuu wa Wilaya. Katika maelekezo yake amewataka viongozi wa wafugaji wa wilaya kuhakikisha zoezi hili linakamilika tarehe 30/03/2022 na endapo matokeo chanya hayataonekana, viongozi wa wafugaji husika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Ameendelea kusema, haoni sababu ya zoezi la kuvalisha mifugo hereni likisuasua wakati wafugaji wote walishapatiwa elimu kuhusu umuhimu wa zoezi hili na viongozi wa wafugaji kitaifa walishiriki kikamilifu katika kuwaelimisha wafugaji hao.
Akisoma taarifa ya zoezi la uvalishaji mifugo hereni mbele ya Mkuu wa Wilaya, Afisa Mifugo Ndg. Emil Mkemwa amesema kwamba, zoezi la uvishaji mifugo hereni lilianza toka tarehe 14/02.2022. Halmasahuri inatarajia kuvalisha hereni Zaidi ya ng’ombe 134,799, mbuzi 159,050, kondoo 80,699 na punda 1,657. Katika taarifa yake hiyo amesema, mpaka kufikia tarehe 12/03/2022 jumla ya mifugo 7,879 (ng’ombe 3,869, mbuzi na kondoo 4,010) imeshavishwa hereni katika kata tatu ambazo ni Toloha, Mgagao na Kigonigoni.
Zoezi la kuvisha mifugo hereni lina faida kubwa kwa wafugaji na Taifa kwa ujumla. Faida zitokanazo na uvishwaji wa hereni ni pamoja na Taifa kupata takwimu sahihi ya mifugo iliyopo, kukabiliana na magonjwa ya mlipuko (chanjo), kurahisisha biashara ya mifugo ndani na nje ya nchi, uthibiti wa wizi wa mifugo na upatikanaji wa mikopo pamoja na bima ya mifugo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa