Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, leo imeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kuhakikisha kwamba, wanatoa mikopo itokanayo na asilimi 10 ya mapato ya ndani, kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Mikopo hiyo, ambayo ina thamani ya fedha za kitanzania Tsh. Milioni 122,767,000/=, imekabidhiwa kwa jumla ya vikundi 15 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Mhe. Salehe R. Mkwizu. Akikabidhi mfano wa hundi ya kiasi hicho cha fedha, Mhe. Mkwizu alisema, fedha hizi ni sehemu ya manufaa ya urejeshaji mzuri unaofanywa na vikundi ambavyo, vikipewa fedha vinarejesha vizuri na kwa wakati.
Mhe. Mkwizu amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuhakikisha kwamba, fedha walizopatiwa wanakwenda kuziingiza kwenye miradi waliyo ombea fedha na siyo kuzifanyia kazi ambayo haikukusudiwa. Pia amewataka kurejesha fedha hizo kwa wakati ili vikundi vingine vikopeshwe, pia nao waendelee kukopeshwa mara nyingi zaidi kadri ya watakavyokuwa wanarejesha.
Akiongea kama sehemu ya msimamizi mkuu wa mikopo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Bi. Mwajuma A. Nasombe, amewaomba Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri kuhakikisha kwamba, wanasimamia vizuri vikundi vyao ili warejeshe mikopo hiyo kwa wakati, ili pia waendelee kukopa zaidi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga imekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Katika mwaka wa fedha wa Serikali 2021/2022, Halmashauri ilifanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Tsh. 481,572,500/= kwa jumla ya vikundi 70.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa