Ikiwa ni siku mbili zimepita baada ya bweni la wasichana wa shule ya Sekondari Nyerere iliyopo Wilayani Mwanga kuungua moto, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe, leo ametoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na pesa taslimu kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi waliounguliwa na vitu vyao vilivyokuwa ndani ya bweni hilo.
Akiongea mbele ya wanafunzi wa shule hiyo, Bi. Nasombe alisema, msaada ambao ameuleta umetokana na ushirikiano mkubwa ulio onyeshwa na watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na timu ya wataalamu wa Halmashauri, Wakuu wa Shule, Waratibu Elimu Kata, Benki, Mheshimiwa Mbunge wa Mwanga pamoja na wadau wengine.
Miongoni mwa vitu vilivyonunuliwa na kukabidhiwa kwa wanafunzi hao ni pamoja na masanduku na kofuli zake zenye thamani ya Tsh. 750,500/=, mafuta ya kujipaka, taulo za kike, ndala, hijabu, vesti, nguo za ndani, masweta na vitu vingine vingi vyenye thamani ya Tsh. 1,270,000/= vya kuwawezesha kuishi maisha kama ya awali ikiwa ni pamoja na kuwapatia fedha taslimu kwa kila mmoja kwa ajili ya fedha za kujikimu katika mahitaji madogo.
Sambamba na michango hiyo, kiasi cha Tsh. 1,020,000/= kilikabidhiwa kwa Mkuu wa Shule hiyo Bi. Severina Mologa kwa ajili ya kuanza ukarabati wa bweni lililoungua. Akikabidhi mchango huo Bi. Nasombe alisema, kiasi hicho ni kianzio tu, kwani Halmashauri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, watahakikisha kuwa bweni hilo linakarabatiwa ndani ya muda na wanafunzi waendelee kulitumia.
Wakati huohuo, Mbunge wa Mwanga Mhe. Tadayo Anania, aliweza kufika shuleni hapo na kutoa jumla ya mifuko 20 ya sementi kwa ajili ya kuunga mkono harakati za kuanza ukarabati. Mhe. Tadayo alisema kwamba, nje ya mchango huo, pia atawaletea madaftari wanafunzi wote waliopatwa na adha ya kuunguliwa na vitu vyao.
Shule ya sekondari Nyerere, bweni lake moja linalotumiwa na wasichana, liliungua moto siku ya jumatano tarehe 14 Septemba, 2022, wakati wanafunzi wakiendelea na masomo majira ya saa tatu asubuhi na kupelekea vitu mbalimbali vya wanafunzi kuungua. Vyombo vya ulinzi na usalama bado vipo kazini kuendelea kuchunguza chanzo cha moto huo, na watakapo maliza kazi yao, taarifa rasmi itatolewa kupitia mamlaka husika.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa