Waziri wa Wizara ya Maji Mhe. Jumaa H. Aweso (Mb) amesema kwamba, Wizara yake itamheshimisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kwamba, mradi wa Same, Mwanga Korogwe unakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kufaidi maji yatakayotokana na mradi huo.
Mheshimiwa Waziri ameyasema hayo leo alipotembelea mradi huo mkubwa wa maji ambao chanzo chake ni bwawa la Nyumba ya Mungu lilipo Wilaya ya Mwanga. Katika maelezo yake amesema, "Mheshimiwa Rais alishanipa maelekezo juu ya mradi huu, nami nasema kwamba, nitahakikisha Wizara yangu inamheshimisha Rais, ili mradi huu uweze kukamilika kwa wakati", alisema Mheshimiwa Waziri.
Pamoja na ziara yake hiyo, Mheshimiwa Waziri ameshuhudia utiaji saini wa mkataba kati ya Wizara na kampuni ya M A KHARAFI AND SONS ya Kuwait, kampuni ambayo imepewa jukumu la kumaliza kazi iliyokuwa imesalia kwa muda wa miezi 14.
Katika kuhakikisha kuwa sehemu ya mradi huo inakamilika ndani ya muda, Mheshimiwa Waziri ametoa maelekezo kwa mkandarasi na kwa wasimamizi wa mradi kutoka Wizarani kuhakikisha kwamba, wanatoa taarifa kila mwezi kwamba mradi umefika asilimia ngapi ya utekelezaji. Ameendelea kusema kwamba, kwa sasa hivi hatarajii kupata visingizio vyovyote kuhusu maendeleo ya mradi kwani fedha zote zilizokuwa zinadaiwa na wakandarasi zimeshalipwa.
Katika hotuba yake, pia amesema kwamba, vijiji vyote tisa vilivyopo katika eneo la chanzo cha maji vitapata maji kwani mpaka sasa usanifu wa kupeleka maji katika vijiji hivyo umeshafanyika.
Akizungumzia suala la ajira kwenye mradi huo, Mheshimiwa Waziri amesema, mbali na kazi zinazohitaji taaluma kwenye mradi, kuna kazi zingine ambazo hazihitaji taaluma, hivyo anatoa wito kwa mkandarasi kuhakikisha kwamba, anatoa ajira kwa vijana wa maeneo ambayo mradi unatekelezwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa