Mtoto Anthony Petro (11) wa Ngara Kagera, leo amekabidhiwa rasmi Wilayani Mwanga Kilimanjaro kwa mfadhili aliyejitokeza kwa ajili ya kumpatia ufadhili wa masomo ambapo atasoma mpaka darasa la saba.
Kabla ya makabidhiano hayo, mtoto Anthony, alipokelewa kwa maandamano yaliyojumuisha wanafunzi wa shule za Mwanga na wananchi wake ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Ndugu Aidan J. Bahama alifanya zoezi la kumkabidhi mtoto huyo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Ndugu Golden A. Mgonzo.
Maandamano ya kumpokea mtoto huyo yalienda mpaka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mwanga ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga alimtambulisha Anthony kwa Mhe. Aaron Y. Mbogho ambaye ni Mkuu wa Wilaya na baadae kuongozana mtoto huyo hadi Ofisi ya Mkurugenzi.
Baada ya zoezi la kumtambulisha na kumkabidhi mtoto huyo kwenye Ofisi ya Mkurugenzi kumalizika, msafara ulielekea shule ya Amani Vumwe English Medium ambapo ndipo alipopatiwa ufadhili wa masomo.
Akizungumza kwa furaha baada ya kukabidiwa mtoto huyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga alisema, mtoto Anthony alikuwa ni mtoto wa maisha ya chini ila sasa yuko juu na akaendelea kumtia moyo kuwa ili azidi kuwa juu zaidi ni lazima ajiamini, awe na hofu ya Mungu, bidii katika kazi na masomo, nidhamu, tabia njema, kuwa na mahusiano mazuri na wenzake. Na endapo Atazingatia haya atazidi kuendelea kuwa juu na hatarudi chini.
Aidha Mkurugenzi baada ya husia wake kwa Anthony, alimkabidhi mtoto huyo kwa Afisa Elimu Msingi Ngd Allan Said na kwa Afisa Ustawi wa Jamii Ndg Alex Kameo na kuwasisitiza kuwa, wahakikishe wanashirikiana na uongozi wa shule ya Amani Vumwe ili mtoto huyo apate malezi mazuri.
Naye Meneja wa Shule ya Amani Vumwe, Ndg Isaka Msuya, akizungumza katika tukio hilo la kumpokea mtoto huyo, alisema, baada ya kumuona mtoto huyo kwenye mitandao ya kijamii alishawishika kumsaidia na ndipo alipochukua jukumu la kumfadhili mtoto Anthony. Ameahidi kumsomesha Anthony mpaka atakapo maliza masomo yake ya elimu ya msingi. Meneja huyo amewaomba wamiliki wa shule zingine kuwa sehemu ya utumishi katika jamii kwa kusaidia kuwasomesha wasiokuwa na uwezo.
Mtoto huyu alianza kupata umaarufu baada ya taarifa zake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zilizokuwa zimeambatana na video inayoelezea maisha halisi anayoishi yeye na familia yake ambapo tarehe 12 machi, 2018 mwandishi wa habari wa Sahara Media, Ndg Shabani Nassibu Nyamukama alitoa taarifa inayoelezea maisha halisi ya mtoto huyo na ndipo alipojitokeza Meneja wa Shule ya Amani Vumwe na kuahidi kumsaidia kielimu. Pamoja na mtoto huyu kuwa ni mdogo kiumri inaonekana ana uwezo mkubwa wa kupambanua mambo na ufadhili ambao ameupata itakuwa ni njia nzuri ya kumuwezesha kusonga mbele kimaisha.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa