Katika hali isiyo ya kawaida, mvua zinazo endelea kunyesha zimeendelea kuleta madhara makubwa Wilayani Mwanga kiasi cha kupelekea wananchi kupata adha mbalimbali. Pamoja ya kwamba mvua hizi zimenyesha maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mwanga, Kata ya Kileo ndiyo kata ambayo imeathirika zaidi kulinganisha na maeneo mengine.
Mvua hizi za masika zimepelekea baadhi ya watu kuhama nyumba zao kutokana na nyumba hizo kujaa maji ama kuzingirwa na maji. Mbali na nyumba kujaa maji, vyoo navyo vimetitia ama kujaa maji kabisa, baadhi ya nyumba zimebomoka na kuanguka, visima vya maji vimejaa na baadhi ya barabara hazipitiki kabisa.
Akiwa kwenye ziara ya kujionea namna mvua zilivyo leta athari kwenye jamii, Mbunge wa Jimbo la Mwanga Mhe, Prof. Jumanne Maghembe ameelezwa na uongozi wa Kata kuwa, kwa sasa kuna baadhi ya shule ambazo zimezingirwa na maji hivyo inakuwa ngumu kwa wanafunzi wa madarasa ya chini kuhudhuria shuleni. Shule ambazo zimeathirika na mvua hizi ni za msingi na Sekondari. Shule za msingi ni pamoja na Muungano, Kituri na Kalimani. Shule za sekondari ambazo zimekumbwa na tatizo hili ni Kifaru na St. Joseph.
Madhara mengine ambayo yametokea ni baadhi ya mashamba yenye mazao kuingiliwa na mafuriko hivyo kupelekea mazao kusombwa ama maji kutuama kwenye mashamba hayo. Akizungumza kuhusu athari za mvua za msimu huu hususani kwenye kilimo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo na Umwagiliaji Ndugu Hassan Mamboleo amesema, wakazi wa maeneo yaliyo athirika wahakikishe wanafanya jitihada za kutunza akiba ya chakula walicho nacho kwani mazao mengi yameharibika na hali hii itapelea upungufu wa chakula hususani kwa wananchi wa Kileo.
Naye Kaimu Afisa Elimu, Idara ya Elimu Msingi Ndg. Iyogo Isuja akiwa anazungumzia athari zilizojitokeza hususani kwenye taaluma alisema, baadhi ya wanafunzi wameshindwa kwenda shule kutokana na miundo mbinu ya barabara kutopitika hali ambayo inapelekea wanafunzi hao kukosa masomo. Mbali na baadhi ya wanafunzi kukosa masomo, pia walimu walio mbali na maeneo ya kazi, wanafika shuleni kwa kuchelewa kutokana na miundombinu kutokuwa rafiki kupitika. Hii inapelekea vipindi vya masomo kuanza kwa kuchelewa hivyo baadhi ya vipindi, hususani vipindi vya asubuhi havifundishwi kutokana na adha ya miundombinu ya barabara kutuama maji.
Katika kuhakikisha hatua za awali zinachukuliwa, ili kuepuka madhara ya mlipuko wa magonjwa, Serikali imeshagawa dawa za kutibu maji ya kunywa na wananchi wa Kata ya Kileo wamesha gawiwa dawa hizo. Serikali inawaasa wananchi wote wa kileo kuendelea kuchemsha maji ya kunywa pamoja na kuhakikisha wanatumia dawa za kutibu maji walizo pewa ili wasipatwe na mlipuko wa magonjwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa