Mbunge wa Jimbo la Mwanga Mh. Jumanne A. Maghembe amewaambia wananchi wa Kata ya Msangeni kuwa, anachukizwa sana na kitendo cha wazazi kukataa kuchangia chakula cha watoto shuleni.
Mheshimiwa Mbunge ameyasema hayo leo alipokuwa kwenye ziara ya kusikiliza kero za wananchi wa Kata ya Msangeni. Akiongea kwa masikitiko alisema, "Nimepata taarifa kuwa, shule ya Sekondari Msangeni wanaokula chakula cha mchana ni wanafunzi sita tu". Ameendelea kusema, hayuko tayari kuona watoto wanashinda na njaa na atahakikisha kuwa mwezi agosti atarudi kukagua ili kuona kama watoto wanakula chakula shuleni.
Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, Mheshimiwa Mbunge amewaagiza watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha kuwa, wanasimamia hili jambo, na kuhakikisha wanakaa na wazazi, na kuwashirikisha ili waone ni kwa namna gani wanaweza kuchangia chakula kwa ajili ya watoto waliopo shuleni.
Pia Mheshimiwa Mbunge ameahidi kuipatia shule ya sekondari Msangeni Kompiuta 45 ambazo zitawasaidia kwenye kujifunza kwa vitendo somo la TEHAMA. Amesema kuwa, hadi kufikia mwezi Octoba, kompiuta hizo zitakuwa zimefika na zitasaidia kuinua taaluma kwenye shule hiyo.
Aidha, Mheshimiwa Mbunge hakuacha kutoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya tano kwa kusema, kwa sasa Serikali imeshafanya mambo mengi na makubwa kwa ajili ya wananchi wa Tanzania. Akitaja baadhi ya miradi mikubwa ambayo Serikali imeshafanya ama inaendelea kufanya ni pamoja na ununuzi wa ndege 7 za abiria, ujenzi wa reli ya kisasa, mradi wa kuzalisha umeme uliopo Selous na ujenzi wa barabara nyingi kwa kiwango cha lami ambapo kwa sasa mikoa mingi imeshaungwanishwa kwa barabara za lami.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa