Mhe. Hamad Hassan Chande (MB) ambaye ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira amefanya ziara katika Ziwa Jipe lililopo Wilayani Mwanga, ziwa ambalo lina ukubwa wa kilomita za mraba 30.
Katika ziara yake hiyo, ameweza kujionea namna ambavyo ziwa hilo lina magugu maji ambayo yamezuia shughuli za kiuchumi kama uvuvi zikifanyika katika ziwa hilo hususani upande wa Tanzania. Akiongea mbele ya viongozi wa wilaya ya Mwanga na wandishi wa habari, Mhe. Naibu Waziri amesema, Serikali haijalala katika kutafuta ufumbuzi wa kuondoa magugu maji katikwa ziwa hilo.
Ameendelea kusema kuwa, Serikali imesha andaa andiko maalum kwa ajili ya kutafuta fedha za kuondoa magugu maji hayo. Amebainisha kuwa, uondoaji wa magugu maji hayo ni sehemu ya mradi mkubwa ambao utahitaji fedha nyingi ili kufanikisha zoezi hilo.
Katika kuhakikisha kuwa mipaka ya ziwa hilo inalindwa na kuwekwa vizuri kwa ajili ya wananchi wa Tanzania, Mhe Naibu Waziri amesema, suala hilo litafanyiwa kazi kwa kuhusisha nchi zote mbili yaani Tanzania na Kenya ili wananchi wa Tanzania wafaidi rasilimali zao. Pia amesema, uongozi wa wilaya ya Mwanga uhakikishe kuwa, unachukua hatua za makusudi kulinda maeneo yanayo zunguka ziwa ili pasiwepo na kilimo kwani kilimo kandokando mwa ziwa panasababisha uharibifu ndani na nje ya ziwa.
Aidha katika ziara yake hiyo, Mhe. Naibu Waziri aliweza kutembelea kiwanda cha Biochem, kiwanda ambacho kinazalisha spiriti kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Akiwa kiwandani hapo, aliweza kukagua maeneo mbalimbali na kuridhishwa namna ambavyo wamiliki wa kiwanda wanajitahidi katika utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kutii maagizo mbalimbali yaliyokwisha tolewa na serikali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mfumo wa maji taka unawekwa vizuri, agizo ambalo wamiliki walishalifanyia kazi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa