Leo Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. David E. Silinde ametembelea na kujionea miradi mitatu inayoendelea kutekelezwa hapa Wilayani Mwanga. Ziara hiyo ameifanya ikiwa ni sehemu ya mikakati ya serikali kuendelea kukagua na kujionea namna utekelezaji wa miradi hiyo unavyo kwenda.
Miradi aliyotembelea ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kisangara – Shighatini wenye thamani ya Tsh. Milioni 617.9, mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Kirya ambao kwa hatua za awali umepatiwa kiasi cha Tsh. Milioni 250 na mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari Kivisini ambao umepatiwa kiasi cha Tsh. Milioni 470.
Katika ziara yake hiyo, Mhe. Naibu Waziri ametoa maelekezo kwa Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mwanga na Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Mwanga kuhakikisha kuwa, wanaisimamia miradi hiyo kwa weledi na umakini mkubwa ili iwe na tija kwa wananchi. Amewataka viongozi hao kusimamia vizuri fedha za Serikali na zifanye kazi iliyo kusudiwa. Akizungumzia suala la ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya, Mhe. Waziri amesema kuwa, serikali ilisha ahidi kutoa fedha hizo na zitakuja muda wowote kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2021/2022.
Akisoma taarifa ya mradi wa Barabara ya Kisangara - Shighatini mbele ya Mhe. Waziri, Mhandisi wa TARURA Wilaya ya Mwanga Ndg. Emmanuel Yohana alisema kwamba, barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 12.3 ujenzi wake umefikia asilimia 47 na itakamilika mwezi juni, 2022.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe amesema kwamba, mradi wa ujenzi wa Kituo cha afya ambao unategemea kunufaisha takribani wananchi 8554 mpaka sasa upo katika hatua ya kupandisha kuta na ameahidi ujenzi utakwenda kwa kasi ili kukidhi matakwa ya serikali. Mkurugenzi ameeendelea kusema, hadi kufikia sasa kiasi cha Tsh. Milioni 43 imesha tumika. Pia amesema katika hatua za kujenga majengo ya kituo hicho cha afya, wananchi wameshiriki kwa kuchangia kiasi cha Tsh. Milioni 6 na wadau wa maendeleo wamechangia kiasi cha Tsh. Milioni 4.2.
Aidha katika mradi wa Kivisini Sekondari, mradi ambao upo katika hatua za kupandisha kuta, Mkurugenzi Mtendaji alisema wananchi wa eneo husika wameshiriki vizuri katika hatua zote toka mradi ulipo anza na wamesha changia kiasi cha Tsh. Milioni 8.7. Aliendelea kusema kwamba, Halmashauri kwa hatua za awali imeweza kufanya manunuzi mbalimbali kutoka kiwandani ili kupunguza gharama za vifaa ambavyo vingeweza kununuliwa kwa bei ya juu kutoka kwenye maduka yasiyo ya jumla.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa