Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amesema kwamba, anaridhishwa na kasi aliyo iona katika ujenzi wa Hospitali Mpya ya Wilaya ya Mwanga.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo jana tarehe 02.05.2023 alipokuwa katika ukaguzi wa miradi Wilayani Mwanga. Akiwa katika eneo la mradi wa Hospitali hiyo, alipokea taarifa fupi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe. Taarifa hiyo ilieleza kwamba, ujenzi wa Hospitali kwa sasa upo katika hatua za umaliziaji kwa majengo ya awamu ya kwanza huku majengo ya awamu ya pili yakiwa katika hatua tofauti.
Nimefurahishwa sana na jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi mkubwa namna hii, alisema Mhe. Mkuu wa Mkoa. Pamoja na pongezi nyingi alizozitoa kwa uongozi wa Wilaya kwa kusimamia mradi huo vizuri, pia ametoa wito kwa viongozi wa Wilaya kuhakikisha kwamba, panakuwepo na usimamizi mzuri wa vifaa vya ujenzi kwa kuhakikisha kwamba ulinzi unakuwepo wa kutosha ili kuepuka upotevu na ubadhirifu kwenye vifaa hivyo.
Pamoja na ziara yake hiyo ya kukagua mradi wa Hospitali mpya ya Wilaya, Mhe. Mkuu wa Mkoa pia alitembelea miradi mitatu ya ujenzi wa barabara. Miradi hiyo ni Ujenzi wa Barabara ya Kisangara – Shighatini (KM 5), Ujenzi wa madaraja 16 katika barabara ya C. D Msuya (KM 13.8) na ujenzi wa barabara ya Kituri Proper (KM 4.2).
Ujenzi wa barabara hizo unatarajiwa kuleta chachu kubwa ya maendeleo kwa wananchi wa Mwanga kwa kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa kuboresha sekta ya usafiri na kurahisisha usafirishaji wa mazao ya wakulima kwa ajili ya biashara, Pia barabara hizo zitarahisisha katika utoaji wa huduma za afya na elimu.
Akisoma taarifa ya miradi hiyo kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa, Meneja wa Mradi wa Wilaya ya Mwanga Ndg. David Msechu alisema kwamba, thamani ya mradi wa barabara ya Kisangara – Shighatini ni Tsh. 513,908,081, mradi wa barabara ya C. D Msuya ni Tsh. 4,999,695,872.00 na mradi wa barabara ya Kituri Proper una thamani ya Tsh. 490,800,500.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa