Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, imeendelea kuneemeka hususani kwenye vituo vya afya ambapo, kwa mara nyingine tena imepatiwa kiasi cha Tsh milioni 400 kwa ajili ya upanuzi wa kituo cha afya Kigonigoni.
Ikumbukwe kuwa na kituo cha afya Kisangara nacho kilipewa idadi ya fedha kama hizo na kituo kipo katika hatua ya kumaliziwa majengo matatu.
Akizungumza ofisini kwake, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya Ndugu Alex Kameo amesema, Kituo cha afya Kigonigoni kimepewa kiasi hicho cha fedha ili kuweza kupanua miundo mbinu yake na kuhakikisha panakuwepo na utoaji wa huduma ya kiwango kizuri kwa jamii. Majengo yatakayo jengwa ni pamoja na; jengo la maabara, jengo la wazazi, jengo la upasuaji na sehemu ya kuchomea taka
Ameendelea kusema kuwa, ili kuhakikisha kazi ya ujenzi inakwenda vizuri na ujenzi unakuwa imara, Mhandisi wa ujenzi Wilaya ndiye atakaye kuwa msimamizi mkuu wa ujenzi huo na kutoa ushauri kwa kila hatua ya ujenzi. Aidha ili kulinda na kuepuka ubadhirifu, kitengo cha manunuzi kitahusika kwenye hatua zote za ununuzi wa vifaa vya ujenzi.
Pia amesema kuwa, kwa mujibu wa muongozo, zimeshaundwa kamati tatu zitakazo husika na usimamizi wa ujenzi wa miundombinu hiyo. Kamati zilizoundwa ni Kamati ya Ujenzi, Kamati ya Manunuzi na Kamati ya Mapokezi. Kamati hizi zitashirikiana na Mhandisi wa Wilaya na Afisa Manunuzi Wilaya kwenye shughuli mbalimbali za ujenzi zitakazokuwa zinafanyika.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa