Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe jana amefanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya elimu na afya katika kata za Mwanga na Kivisini na kujionea namna ujenzi wa miradi hiyo unavyokwenda. Katika ziara yake hiyo, Bi. Nasombe amefurahishwa kwa kuona miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali huku mingine ikiwa imesha kamilika.
Katika Kata ya Kivisini, Mkurugenzi aliweza kutembelea eneo ambalo shule mpya ya sekondari ya Kivisini inajengwa, pia alifika na kuona mradi wa zahanati ya kijiji cha Kitoghoto pamoja na ofisi ya kijiji cha Kitoghoto.
Mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari Kivisini umepatiwa kiasi cha fedha za kitanzania milioni 470 na mara mradi huu utakapokamilika utakuwa na tija kubwa kwa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba katika kata ya Kivisini na kata za jirani pamoja na Wilaya ya Mwanga kwa ujumla. Aidha, mradi wa zahanati ya kijiji cha Kitoghoto ni mradi ambao upo katika hatua ya umaliziaji. Mradi huu umeshapatiwa kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 50 ili uweze kukamilika na kuanza kutumika. Mradi mwingine ambao Halmashauri imeupatia fedha kwa ajili ya kuuendeleza ni mradi wa Zahanati ya Kitoghoto, mradi umepatiwa kiasi cha shilingi milioni 13 za mapato ya ndani na shilingi milioni 5 kutoka kwenye mfuko wa jimbo wa ofisi ya Mbunge wa Mwanga.
Mradi mwingine alioweza kutembelea Mkurugenzi ni mradi wa ujenzi wa madarasa matatu na ofisi moja katika shule ya Sekondari Mandaka. Mradi huu una thamani ya fedha kiasi cha milioni 60 na umesha kamilika.
Mkurugenzi wa Mwanga amekuwa na utaratibu wa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo kwa lengo la kujionea na kujiridhisha kama miradi hiyo inakwenda vizuri pamoja na kujionea changamoto zilizopo ili serikali iweze kukabiliana nazo kwa wakati. Hata hivyo, ameendelea kufurahishwa kwa namna miradi inavyokwenda vizuri na kwa kasi inayo ridhisha.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa