Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kiasi cha fedha Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe katika Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Teacher Resource Centre (TRC). Amesema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imeridhia kutenga kiasi hicho kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Halmashauri kwa sasa inakuwa na jengo la utawala kwani jengo linalotumika sasa ni jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Sambamba na hilo, Mkurugenzi amesema kuwa, serikali pia imeridhia kutoa kiasi cha shilingi Bilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali mpya ya Wilaya, hospitali ambayo si kwamba itakuwa mkombozi kwa wana mwanga tu, bali hata wilaya jirani zinazo izunguka wilaya ya Mwanga zitanufaika na ujenzi wa hospitali hiyo.
Akizungumzia suala la mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Mkurugenzi amesema kwamba, Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga mpaka sasa imefanikiwa kutoa mkopo kwa vikundi 48, mkopo wenye thamani ya Tsh. Milioni 269.8 kwa makundi yote matatu. Mikopo hii imetokana na jitihada kubwa iliyofanywa na Halmashauri katika kukusanya mapato ya ndani ambapo hadi kufikia kipindi cha robo ya pili 2021/2022 Halmashauri imefanikiwa kukusanya kiasi cha Bilioni moja na milioni miambili ishirini na moja. Ukusanyaji wa mapato ya ndani umekuwa ni chachu kubwa katika kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo, kwa mwaka huu wa fedha Milioni 344 imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ya Wilaya.
Aidha, Mkurugenzi amewashukuru Waheshimiwa Madiwani kwa ushirikiano wao mzuri walio uonyesha katika uanzishwaji wa mradi wa kimkakati wa Halmashauri, mradi wa kufyatua matofali. Akielezea manufaa ya mradi huo ambao ulianza kufanya kazi mwezi octoba 2021, Mkurugenzi alisema kuwa, mpaka kufikia sasa mradi umesha zalisha jumla ya matofali 62,178 na kufanikiwa kuingiza kiasi cha Tsh. Milioni 92. Amesema, mradi unaendelea vizuri na ameendelea kuomba Waheshimiwa madiwani pamoja na wananchi kuendelea kuunga mkono mradi huu kwa manufaa ya Halmashauri ya Mwanga na wananchi wake.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa