Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kiasi cha Tsh. 584,280,028/= kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Toloha.
Akitambulisha mradi huo kwa wananchi wa Kata ya Toloha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe aliwaambia wananchi hao kwamba, mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa na ya kimkakati ndani ya Halmashauri ya Mwanga.
Mkurugenzi aliwaambia wananchi hao kwamba, Serikali imedhamiria kujenga shule hiyo kwa kasi, ili ujenzi ukamilike mapema na watoto wa Toloha pamoja na watanzania wengine waweze kufaidi matunda ya serikali, inayo ongozwa na Rais Dr. Samia Suluhu Hassan.
Naye msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Agrey Mawole aliwaambia wananchi hao kwamba, miundombinu itakayojengwa kwenye shule hiyo ni pamoja na ujenzi wa madarasa nane, chumba cha computer, maabara ya kemia, fizikia na biolojia. Miundombinu mingine ni ujenzi wa jengo la utawala, maktaba, matundu 20 ya vyoo, mnara wa tenki la maji, sehemu ya kunawia mikono na mashimo ya maji taka pamoja na mifumo yake.
Wakati huohuo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, aliwajulisha wananchi wa Kata ya Kivisini kwamba, Serikali imeleta fedha kiasi cha Tsh. 98,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mpya ya mwalimu (Two in One).
Fedha za ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Toloha pamoja na ujenzi wa nyumba ya mwalimu Kivisini Sekondari ni fedha zilizoletwa na Serikali kupitia mradi wa Secondary Education Quality Improvement Project (SEQUIP).
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa