Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (TASAF), imeipatia shule ya Msingi Mwero iliyopo kata ya Kirongwe fedha za kitanzania shilingi milioni 178,392,857.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwero, jana tarehe 11.10.2023, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe amewaambia wananchi hao kwamba, serikalai imeleta fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya mawili, vyoo matundu 6, nyumba ya watumishi wawili (2 in 1) na ofisi moja.
Mkurugenzi Mtendaji amewataka wananchi wa kijiji hicho kuhakikisha kwamba, wanatoa ushirikiano kwenye mradi huo mara utekelezaji wake utakapo anza. Amewaambia kwamba, wananchi wanapaswa kuchangia asilimia kumi kwenye mradi na asilimia hii itakuwa ni pamoja na kuchangia vifaa vya ujenzi na nguvu kazi zao.
Naye Afisa Ufuatiliaji wa TASAF Wilaya ya Mwanga Ndugu Joseph Elieza, aliwaeleza wananchi wa Kijiji hicho kuwa, Mwero imepata bahati ya kipekee kuupata mradi huu, hivyo wanapaswa kutoa ushirikiano wakati wa ujenzi na kuhakikisha kuwa mradi huo unalindwa na kutunzwa vizuri mara utakapo kamilika. Pia amewahakikishia wananchi hao kuwa, mradi huo utakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.
Aidha Diwani wa Kata ya Kirongwe, Mhe. Sarumbo Mkono, ameishukuru Serikali kwa kuweza kuwaletea mradi huo kwani, mradi huo umekuja kwa wakati muafaka. Ameahidi kutoa ushirikiano yeye na wananchi wake kwa kujitoa wakati wote ili mradi huo ukamilike kwa wakati na uweze kuwanufaisha wananchi pamoja na watotom wao.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa