Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imetoa shukrani kwa uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha kwa kugawa chakula bure kwa wananchi wa vijiji saba wilayani Mwanga.
Shukrani hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Bi. Mwajuma A. Nasombe ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mwanga kwenye zoezi hilo la kugawa chakula.
Akitoa shukrani zake kwa kanisa hilo, Bi. Nasombe amesema, analishukuru sana kanisa la KKKT na viongozi wake kwa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha kwamba, kanisa linashirikiana na serikali katika kukabiliana na tatizo la njaa. Katika shukrani zake hizo, pia ameishukuru serikali kwa kuleta tani 411 za mahindi ambazo zimeuziwa wananchi wa Mwanga kwa bei nafuu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Kanisa la KKKT, Mhe. Baba Askofu wa Dayosisi ya Mwanga, Chedieli E. Sendoro, amesema, anaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kuwapa ushirikiano katika masuala mbalimbali pale kanisa linapohitaji msaada.
Pamoja na shukrani hizo, Mhe. Baba Askofu ameongoza zoezi la ugawaji wa vyakula mbalimbali kwa wananchi wa Kata ya Toloha. Katika hotuba yake amesema kwamba, msaada walioutoa haujaishia Toloha tu, bali umejumuisha jumla ya vijiji saba ambavyo ni Pangaro, Kiverenge, Karambandea, Simu Kizungo, Kwakoa, Kwakihindi na Kwanyange. Amesema kwamba, jumla ya Kaya 780 zimenufaika na msaada wa vyakula mbalimbali ikiwa ni tani 39 za mahindi, tani 15 za maharage, tani 8 za unga wa lishe na lita 3300 za mafuta ya kula.
Serikali Wilayani Mwanga, imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na mashirika pamoja na taasisi mbalimbali za umma na binafsi kwa manufaa ya kuhakikisha kwamba, wananchi wake, wanapata huduma muhimu na za msingi haswa za kibinadamu.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa