Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe amesema kuwa, hajaridhishwa na utendaji kazi wa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kisangara na Mtunza stoo wa kituo hicho. Ameyasema hayo leo alipotembelea kituo hicho ikiwa ni mara yake ya pili kufika hapo baada ya kutembelea tena tarehe 17 Septemba, 2021.
Kitendo cha kutoridhishwa na utendaji wa watumishi hao, imepelekea Mkurugenzi Mtendaji kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi juu ya mapungufu ya awali yaliyobainika katika kituo hicho. Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa, tarehe 17 septemba, 2021 alifika katika kituo hicho na kubaini kuwa, kuna mambo mengi yasiyoridhisha kwenye mapokezi, utunzaji na utoaji wa dawa kwa ajili ya wagonjwa, wagonjwa kununua dawa/vifaa tiba nje wakati dawa zipo kituoni, baadhi ya dawa zikitoka stoo hazifiki katika chumba cha kutolea dawa ikiwa ni pamoja na chumba cha kutolea dawa kuwa na watoaji huduma wengi kinyume na taratibu.
Aidha, baada ya Mkurugenzi Mtendaji kubaini dosari zilizopo katika kituo hicho, tarehe 18 septemba, 2021 aliunda timu ya wataalamu sita kwa ajili ya kwenda kufanya uchunguzi kituoni hapo ambapo, kwa uchunguzi wa awali imebainika kuwa, kuanzia mwezi julai, 2020 hadi tarehe ya ukaguzi (18/09/2021) kituo kilinunua dawa zenye thamani ya Tsh. 19,693,898.16 ambapo katika fedha hizo, dawa zenye thamani ya Tsh. 3,134,500 hazikuingizwa kwenye leja, pili, kukosekana kwa jalada la nyaraka za mapokezi ya dawa, tatu, menejimenti kutozingatia miongozo juu ya kuingiza bidhaa katika leja kabla ya kufanya matumizi na nne, kukosekana kwa mtu sahihi juu ya utunzaji wa nyaraka za mapokezi ya kituo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwanga ambaye alifika Wilayani Mwanga mwezi Agosti, 2021, amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri kwa ajili ya kujionea namna ambavyo watumishi wanawajibika katika kutoa huduma kwa wananchi na serikali yao. Pia amekuwa akitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo mingi inatekelezwa na fedha kutoka serikalini, wahisani na wananchi. Ziara kama hizi zimekuwa na manufaa kwa Halmashauri kwani inasaidia kubaini changamoto ambazo zipo na namna ya kukabiliana nazo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa