Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga siku ya leo imeungana na wanawake kote Ulimwenguni kuadhimisha siku ya Wanawake ambayo huadhimishwa tarehe 08 Machi, 2018 kila mwaka. Maadhimisho hayo yamefanyika Mamlaka ya Mji Mdogo Mwanga na kuweza kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo watumishi na wananchi.
Wakisoma risala yao mbele ya Mgeni Rasmi ambaye alikuwa ni Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Ndg Aaron Yesaya Mmbogho, wanawake hao walisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa mitaji, ukatili dhidi ya wanawake, kudhulumiwa mali, kutoshirikishwa katika kutoa maamuzi katika mali zinazozalishwa na familia sambamba na uwepo wa baadhi ya mila gandamizi.
Wanawake hao waliendelea kusema pamoja na changamoto mbalimbali walizo nazo siku ya leo wameweza kujitolea kwa kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum wanaosoma shule ya Msingi Mavusha kwa kuwapatia zawadi mbalimbali zenye thamani ya shilingi 250,000/=.
Maadhimisho hayo ambayo yalibebwa na kauli mbiu “Kuelekea Uchumi wa Viwanda Tuimarishe Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake Vijijini” yaliambatana na zoezi la kutoa cheki za mikopo kwa vikundi vinne vya wanawake wajasiriamali ambapo kiasi cha shilingi 10,000,000/= kilitolewa leo.
Akitoa hotuba yake kwa wanawake Mhe. Mkuu wa Wilaya alisema katika kuelekea uchumi wa viwanda na kuimarisha usawa wa kijinsia Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kwa mwaka wa fedha 2016/17 imetoa mikopo kiasi cha shilingi 34,000,000/= kwa vikundi vya wanawake vipatavyo kumi na kwa mwaka wa fedha 2017/18 hadi kufikia leo kiasi cha shilingi 25,000,000/= tayari zitakuwa zimekwisha tolewa kwa vikundi vya wanawake. Aliendelea kusisitiza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo sisi kama jamii tunalo jukumu la kuadhimisha siku hii ili kutathmini mafanikio na changamoto zinazowakabili wanawake katika kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake waliopatiwa mkopo leo Bi. Fotunata P. Mruma wa kikundi cha Tumaini kinachotokea Kata ya Kilomeni alisema Halmashauri imeweza kuwatoa kwenye hatua moja kwenda hatua nyingine nzuri zaidi. “ Tunaishukuru sana Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii kwani mitaji tuliyopata itatusaidia kununua chakula cha kuku na madawa hivyo uzalishaji utaongezeka na biashara itakuwa” alisema Bi. Fotunata.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa