Ikiwa kama sehemu ya kuendeleza michezo Wilayani Mwanga, leo ilikuwa siku ya kuhitimisha michezo ya Habibu Cup, michezo ambayo inafadhiliwa, kusimamiwa na kuendeshwa na Taasisi ya Elimu ya Green Bird ya hapa Mwanga.
Lengo kubwa la michezo hii ambayo huu ni mwaka wake wa tano ikifanyika ni kumuenzi muasisi wa Taasisi ya Elimu Green Bird, Mzee Habibu Mndeme ambaye kwa jitihada zake aliweza kuianzisha taasisi hiyo kwa lengo la kutoa elimu kwa watanzania.
Michezo hii kwa mwaka huu ilianza januari, 2018 ambapo jumla ya shule 18 za sekondari zilishiriki na vyuo 4 navyo vilishiriki. Michezo iliyokuwa inachezwa ni mpira wa miguu, mpira wa netiboli na riadha ambayo imefanyika leo siku ya fainali. Timu ambazo zilifanikiwa kuingia fainali kwa mpira wa miguu ni Green Bird High School na Green Bird College. Kwa upande wa netiboli timu zilizofuzu kuingia fainali ni Usangi Day Sekondari na Green Bird College. Hata hivyo baada ya fainali kuchezwa timu ya Green Bird College waliibuka washindi kwa upande wa mpira wa miguu na kuweza kukabidhiwa kombe na kitita cha Tsh 1,500,000= ambapo mshindi wa pili alipewa kiasi cha Tsh. 750,000=. Kwa upande wa netiboli timu ya Green Bird College iliibuka na ushindi na kukabidhiwa kombe na kiasi cha Tsh. 800,000= na mshindi wa pili alikabidhiwa Tsh. 400,000=.
Michezo hii imekuwa ya manufaa sana kwa wanafunzi, kwani imekuwa ikiibua na kuendeleza vipaji kwa wanafunzi wengi ambapo vipaji vyao vinakuwa ni hazina kwao binafsi na Taifa kwa ujumla. Pia imekuwa na manufaa makubwa ndani ya wilaya kwani wanafunzi wengi wanaoshiriki michezo hii wamekuwa wakipata nafasi kubwa, ya kushiriki michezo ya UMISSETA, michezo ambayo huwa inashirikisha wanafunzi kunzia ngazi ya Shule, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa. Pia michezo hii imekuwa ikitoa burudani kwa wananchi wa mwanga hususani kwa wapenzi wa michezo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa